Huko Mtibwa mambo ni moto, wachezaji wapewa sharti la kuzifyeka Simba, Yanga

Muktasari:

Kocha huyo alisema kuondoka ondoka kwa wachezaji wake muhimu kumemlazimisha kukijenga upya kikosi chake karibu kila msimu.

Dar es Salaam. Kocha wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila amezionya Simba na Yanga kuwa safari hii zitaambulia patupu kwani kuna mkakati wameuandaa ili kuhakikisha nyota wa kikosi hicho wanasalia kwenye klabu hiyo.

Katwila alisema anataka kuhakikisha wachezaji wake muhimu wanabaki kwenye kikosi chake ili waje kivingine msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2019/20.

Kocha huyo alisema kuondoka ondoka kwa wachezaji wake muhimu kumemlazimisha kukijenga upya kikosi chake karibu kila msimu.

“Kubaki na wachezaji wangu muhimu ina maana kazi itakuwa ndogo ya kuboresha maeneo machache ambayo msimu huu yamekuwa ni changamoto kwetu,” alisema kocha huyo.

Mtibwa Sugar wenye pointi 49 katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, watakuwa na kibarua kizito leo kwenye uwanja wa Mkwakwani, Tanga kucheza dhidi ya wenyeji wao, Coastal Union.