Emery: Kipigo cha 3-1 hakitukwamishi kufuzu Ligi ya Mabingwa mwakani

Muktasari:

Mabao ya Wolves ambao wamekuwa wababe kwa vigogo wa Top Six msimu huu, yalipachikwa na Ruben Neves, Matt Doherty na Diogo Jota.

Kocha wa Arsenal, Unai Emery amesema licha ya kupoteza mchezo wake muhimu dhidi ya Wolves kwa kuchapwa mabao 3-1 lakini bado anamatumaini ya kumaliza kwenye nafasi nne za juu.

Emery anaamini mipango yake ya kumaliza nafasi nne za juu itaiwezesha timu hiyo kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Arsenal ambao walisafiri hadi kwenye dimba la Molineux kuikabili Wolves, walikutana na kipigo cha aibu kwa kupigwa mabao 3-1.
Arsenal imekutana na kipigo hicho ikitoka kuchapwa mabao 3-2 na Crystal Palace kwenye dimba lake la nyumbani, Emirates.
Mabao ya Wolves ambao wamekuwa wababe kwa vigogo wa Top Six msimu huu, yalipachikwa na Ruben Neves, Matt Doherty na Diogo Jota.
Katika mechi nyingine ambayo ilikuwa ikisubiriwa na mashabiki wengi, kama ilivyotarajiwa na wengi kwamba, Man City ilikuwa inakwenda kupata ushindi kwenye mchezo huo, huku mashabiki wa Man United wakiweka bayana kwamba, haitawauma hata kama watapoteza mchezo huo.
Matokeo hayo yameiweka Man City kileleni ikiwa na alama 89 huku ikifuatiwa na Liverpool wenye pointi 88 na ambao, jana walikuwa wakiishabikia Man United kwa muda ili wawachape wapinzani wao hao kwenye mbio za ubingwa msimu huu. Kipindi cha kwanza, timu zote zilicheza kwa kushambuliana kwa zamu huku Man City wakionekana kumiliki zaidi mpira, lakini hadi mapumziko matokeo yalikuwa sare.
Kipindi cha pili, kiliwachukua Man City dakika tisa kupata bao la kuongoza kupitia kwa Bernado, baada ya shuti lake kumshinda kipa David De Gea.
Bao hilo liliifanya Man United kufunguka kujaribu kupata bao la kusawazisha, lakini wakati wakiendelea kupambana Sane aliyeingia kuchukua nafasi ya Fernandinho, alimaliza shughuli kwa kupachika bao la pili kwa shuti kali akiitendea haki pasi ya Raheem Sterling.
Ushindi huo wa Manchester City umeendelea kutanua rekodi mbovu ya Man United msimu huu, ambapo jana imepoteza mchezo wa sita mfululizo kwenye mechi tisa za karibuni. Pia, umeifanya City kuboresha rekodi zake kwa kufunga bao la 157 kwenye mashindano yote msimu ikivunja rekodi yake yenyewe iliyoiweka msimu wa 2013/14.