Ada, Ng’anzi Serengeti wanatakiwa kutunzwa

KIUNGO wa Lipuli ya Iringa, Shaaban Ada ambaye alikuwa katika kikosi cha Serengeti Boys kilichokwenda kushiriki fainali za Mataifa Afrika (Afcon) nchini Gabon 2017, alisema timu hii ya sasa inatakiwa kutunzwa ile kuleta matunda zaidi.

Ada alisema katika timu yao takribani wachezaji wote waliokwenda Gabon walikuwa na uwezo na vipaji lakini tangu walivyoshindwa kufuzu kwenda kucheza kombe la dunia waligawanyika na kila mmoja kwenda kutafuta maisha ya soka katika timu nyingine.

Alisema hata Serengeti Boys ya wakati huu wanatakiwa kutunzwa na kuwekwa pamoja ili kuwa na muendelezo mzuri ambao watakuja kucheza timu za Taifa za umri mwingine mpaka kufika Taifa Stars.

“Nimeliona hilo kutoka timu yetu mbali ya kuwa na wachezaji ambao walionekana kuwa vizuri tena katika misingi ya soka lakini sasa hivi kila mmoja yupo katika timu yake na hatuna tena ule muendelezo wa kukutana kama ilivyokuwa hapo awali,” alisema.

Ally Ng’azi ambaye nae alikuwa katika kikosi hiko cha Serengeti Boys kilicho kwenda Gabon alisema wao kizazi chao kupotea mbali ya kuonekana kuwa na wachezaji wengi ambao walikuwa na uwezo ni kubweteka na kile ambacho walikipata baada ya kwenda kushiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza.

“Serengeti Boys ya sasa wachezaji kwanza wanatakiwa kujitambua wenyewe na si kubweteka baada ya kupiga hatua hiyo, lakini Serikali na Shirikisho la soka Tanzania (TFF) wanatakiwa kuwaendeleza na kuwatunza zaidi ya wakati huu wanaweza kuwa faida kwa nchi siku za usoni kwani wengi wao wanauwezo wa kucheza mpira,” alisema Ng’anzi.