Hesabu za vidole kwa Watanzania Serengeti Boys ikitupa kete ya mwisho

Muktasari:

Serengeti Boys inahitajika kuibuka na ushindi wa angalau mabao 4-0 dhidi ya Angola kwenye mchezo wa mwisho huku ikiombea Nigeria iifunge Uganda mabao kuanzia 3-0 ili iweze kupenya na kufuzu nusu fainali.

Dar es Salaam. Matumaini kwa Watanzania juu ya uwezekano wa Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 'Serengeti Boys' kufuzu hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Afrika kwa vijana wenye umri huo (AFCON U17) yanayoendelea nchini yamefifia.
Kipigo cha mabao 3-0 kwenye mechi ya pili dhidi ya Uganda juzi Jumatano, kimeifanya Serengeti Boys kuwa kwenye nafasi finyu ya kutinga nusu fainali pamoja na kujihakikishia tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia kupitia kundi A kwani inashika mkia ikiwa haina pointi, ikifungwa mabao nane na kufunga mabao manne.
Serengeti Boys inahitajika kuibuka na ushindi wa angalau mabao 4-0 dhidi ya Angola kwenye mchezo wa mwisho huku ikiombea Nigeria iifunge Uganda mabao kuanzia 3-0 ili iweze kupenya na kufuzu nusu fainali.
Hata hivyo hilo la kutegemea miujiza hiyo inayohitajika ya mechi ya mwisho lisingetokea ikiwa Serengeti Boys ingepata ushindi au kutoka sare na Uganda kwenye mchezo wa juzi ambao Watanzania wengi walikuwa na imani na matumaini makubwa kuwa ingeweza kuwatoa kimasomaso.
Mwanaspoti linakuletea tathmini ya mchezo wa juzi ambao Serengeti ilichapwa mabao 3-0 na dondoo nyingine muhimu za kinachoendelea kwenye mashindano hayo.
Viungo, Mabeki donda ndugu
Kama Serengeti Boys itayaaga mashindano hayo, hakuna namna unayoweza kukwepa kushusha lawama kwa benchi lake la ufundi kwa kushindwa kuandaa safu imara ya kiungo na ulinzi jambo ambalo limeigharimu timu katika mechi mbili za mwanzo.
Kwenye mchezo wa juzi dhidi ya Uganda, timu ilionekana kukosa mawasiliano na muunganiko mzuri ndani ya uwanja jambo ambalo lilichangiwa na udhaifu wa safu ya kiungo iliyoelemewa sehemu kubwa ya mchezo.
Udhaifu huo wa safu ya kiungo uliwafanya Uganda kutawala mchezo na kuziba njia za washambuliaji wa Serengeti Boys kupata mipira huku ikitengeneza nafasi za mabao ambazo zilizotumiwa vyema na washambuliaji wake.
Mbaya zaidi, safu ya ulinzi ya Serengeti Boys ilizidi kuongeza ukubwa wa tatizo kwa kufanya makosa mengi ya mchezaji mmoja mmoja ambayo yalikuwa faida kwa wapinzani.

Benchi la ufundi lijitafakari
Matatizo ya Serengeti Boys yalianza kuonekana tangu dakika za mwanzo za mchezo lakini benchi lake la ufundi chini ya Oscar Mirambo lilionekana kushindwa kufanya mabadiliko ya haraka ya kimbinu ambayo yangeweza kuiokoa na aibu iliyoikuta.
Uganda walionekana kuwa imara katikati na Serengeti Boys ililazimisha kupenya kupitia hapohapo wakati nguvu yake ilionekana kuwa pembeni.

Mirambo na benchi lake walipokuja kushtuka na kubadili mbinu, muda ulikuwa umeshakaribia ukingoni na Uganda tayari walikuwa wamshamaliza mchezo kutokana na mabao yao matatu.

Angola darasa tosha
Kama kuna timu ambayo inapaswa kuwa mfano mzuri kwa wachezaji na makocha wa Serengeti Boys na Watanzania kwa ujumla basi ni ile ya vijana ya Angola.
Inacheza soka la mbinu na nidhamu kubwa ikiwa inashambulia na kuzuia kwa uwiano mzuri ambao hauiweki kwenye hatari kubwa kwenye mchezo.
Angola ni timu ambayo imeonyesha uwezo mkubwa wa kuisoma na kuiheshimu timu pinzani na mfano wa hilo ni namna ilivyocheza na Nigeria ambapo iliwapa heshima wapinzani kwa kuwaruhusu wamiliki mpira huku ikiziba mianya ya kuingia kwenye eneo lao la hatari na kisha kushambulia kwa hesabu.
Matokeo yake ilijikuta ikifungwa bao 1-0 tu huku ikicheza pungufu kwa muda mrefu wakati katika mechi ya kwanza dhidi ya Serengeti Boys iliyokuwa kamili, Nigeria ilipata ushindi wa mabao 5-4.

Abraham ana mkosi gani?
Mmoja wa nyota ambao alikuwa anatabiriwa kufanya vizuri kwenye mashindano hayo ni nahodha wa Serengeti Boys, Morice Abraham kutokana na uwezo mkubwa wa kuchezesha timu, kuvunja ukuta wa timu pinzani na kufunga mabao.
Hata hivyo mambo yamekuwa tofauti na nahodha huyo amekuwa miongoni mwa wachezaji ambao wamechemesha kwenye mashindano hayo hadi sasa.
Baada ya kutamba kwenye mashindano mengi tofauti, Morice amekuja kufanya vibaya kwenye mashindano ambayo yanavutia kundi kubwa la mawakala, inasikitisha kwakweli.