Senegal yategemea mbeleko ya Cameroon kukata tiketi Brazil

Muktasari:

Ushindi wa mabao 2-1 ambao Guinea imeupata dhidi ya Senegal umeifanya ifikishe pointi tatu zinazoiweka kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa kundi B

Dar es Salaam. Wakati Cameroon ikikata tiketi ya kufuzu hatua ya nusu fainali na kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia la vijana wenye umri chini ya miaka 17, hali imekuwa tete kwa Senegal baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Guinea, inategemea miujiza ili iweze kusonga mbele kwenye mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON U17) yanayoendelea nchini.

Kipigo hicho walichokipata kutoka kwa Guinea kimeifanya Senegal ilazimike kuibuka na ushindi kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Cameroon huku ikiombea Guinea na Morocco zitoke sare ili yenyewe iweze kusonga mbele kupitia kundi hilo.

Ushindi wa aina yoyote ambao Guinea wataupata dhidi ya Morocco kwenye mechi ya mwisho maana yake utaifanya Senegal itupwe nje ya mashindano hayo ambayo kabla hayajaanza ilikuwa ni miongoni mwa timu zilizokuwa zikipewa nafasi kubwa kutwaa ubingwa.

Hata hivyo pamoja na ugumu walionao kufuzu hatua ya nusu fainali, wanaamini kitendo cha Cameroon kuwa tayari imeshafuzu hatua hiyo, kitawafanya wapate urahisi kwenye mechi baina yao.

"Kama tunaweza kutengeneza nafasi maana yake tuna uwezo wa kufunga. Mechi ya mwisho tutacheza na Cameroon ambayo kuna uwezekano ikapumzisha wachezaji jambo ambalo linaweza kutupa faida. Jambo la msingi ni kutokata tamaa na kupambana hadi mwisho.

“Katika hoteli tutakaa kikao na wachezaji na kuwakumbusha umuhimu wa kupata ushindi kwenye mchezo wa mwisho," alisema Daf

Kocha wa Guinea, Mohammed Camara alisema matokeo hayo yamewapa molali ya kuelekea mchezo wa mwisho dhidi ya Morocco.

"Jambo la msingi kwenye hiyo mechi ni kwenda kusaka ushindi tu na sio vinginevyo na tunaamini mechi itakuwa ngumu kwa sababu Morocco ni timu nzuri na ngumu," alisema Camara.