Rangi nyekundu yawapa mashabiki Morocco

Muktasari:

Mechi ya Kundi B kati Morocco na Senegal  umemalizika kwa sare 1-1 na kuifanya Cameroon  kuongoza kundi baada ya kuichapa Guinea mabao 2-0.

Dar es Salaam. Kikosi cha Morocco kimepata mashabiki wengi katika mchezo wao na Senegal kutokana na jezi za rangi nyekundu walizovaa.

Mchezo wa Morocco na Senegal unaopigwa Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam ni wa fainali za vijana chini ya miaka 17, AFCON zilizoanza kutimua vumbi Aprili 14 na kumalizika Aprili 28.

Ni kutokana na aina ya jezi za rangi nyekundu walizovaa ambazo huvaliwa na Simba katika mechi zao hasa za nyumbani.

Jezi hizo ni tisheti za rangi nyekundu zenye maandishi meupe na bukta za kijani zenye ufito mweupe na kufanya rangi nyekundu ionekane kwa wingi.

Wapinzani wao Senegal wamevaa jezi za rangi nyeupe zenye ufito wa rangi ya kijani.

Sehemu kubwa ya mashabiki waliopo uwanjani hapa hasa wa jukwaa la upande wa kushoto kutoka meza kuu, wamekuwa wakiimba na kushangilia kwa nguvu Morocco, Morocco.

Wapo wachache walianza kushangilia Senegal lengo kiwapinga wa Morocco kutokana na ushabiki wa Simba na Yanga, lakini sauti zao zilipungu kadri muda ulivyozidi.

Hata hivyo, licha ya sehemu kubwa ya mashabiki ambao wanaaminika ni Watanzania kuwashangilia Morocco, yupo Mtanzania Simon Msuva anacheza Ligi Kuu ya Morocco.