Emery aanza kujuta kumpoteza Ramsey

Muktasari:

Shida iliyomwondoa Ramsey kwenye kikosi cha Arsenal ni kushindwa kuafikiana juu ya mazungumzo ya mkataba mpya upande wa mshahara ambapo Juventus wamekubali kumpa staa huyo Pauni 400,000 kwa wiki na kwenda kuwa mmoja wa wachezaji wanaolipwa pesa ndefu kwenye Serie A

London, England. Kocha, Unai Emery amekiri kujutia kitendo cha mabosi wa Arsenal kushindwa kumbakiza kiungo wake Aaron Ramsey uwanjani Emirates.
Staa huyo wa kimataifa wa Wales mwisho wa msimu huu atakwenda zake kujiunga na Juventus bure kabisa baada ya mkataba wake kufikia tamati huko Arsenal. Lakini, kocha Emery alisema bado anataka kuendelea kumfurahia Ramsey kwenye kikosi ambapo juzi Alhamisi aliisaidia timu hiyo kuichapa Napoli 2-0 katika robo fainali ya kwanza ya Europa League.
Emery alisema mchezaji huyo ataanza pengo kubwa msimu ujao atakapoondoka baada ya mkataba wake kufika tamati Juni. Shida iliyomwondoa Ramsey kwenye kikosi cha Arsenal ni kushindwa kuafikiana juu ya mazungumzo ya mkataba mpya upande wa mshahara ambapo Juventus wamekubali kumpa staa huyo Pauni 400,000 kwa wiki na kwenda kuwa mmoja wa wachezaji wanaolipwa pesa ndefu kwenye Serie A.
"Kiwango chake anachokionyesha kwa sasa bila ya shaka anataka kutufanyia kitu kimoja muhimu. Anataka kutusaidia kufanya kitu fulani kwa sababu anahisia na Arsenal na anawapenda mashabiki wake," alisema Emery.
"Anatupatia kila kitu si kwa ajili yake bali kwa ajili ya klabu. Binafsi nataka niendelee kumfurahia tu kwa sasa. Nataka kufanya kitu fulani muhimu tukiwa naye. Kwa sasa akili yake ipo kwenye kufanya jambo kubwa na Arsenal."