Jeuri ya Pesa: Simba yakwea pipa kuifuata TP Mazembe

Muktasari:

Simba inahitaji sare ya mabao yoyote au kushinda ili kusonga mbele kwa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa baada ya mchezo wa kwanza wa robo fainali kumalizika kwa suluhu jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Jeuri yake kusudi! Ndicho walichofanya Simba baada ya kuwajibu TP Mazembe kwa kuamua kusafiri na ndege kukodi Alfajiri ya leo kuelekea Lubumbashi, Dr Congo tayari kwa mchezo wao wa marudiano utakaopigwa kesho (Jumamosi).

TP Mazembe ilipokuwa nchini wiki iliyopita ilikuja na ndege ya mmiliki wao, lakini leo Bilione wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ amejibu mapigo kwa timu hiyo kwenda na ndege Lubumbashi.

Kikosi hiko kiliondoka katika Uwanja wa ndege wa Terminal One wakiwa na ndege yao binafsi ambayo inaenda moja kwa moja mpaka Lubumbashi.

Akiwa Uwanja wa ndege kabla ya kuondoka, Kocha mkuu wa Simba, Patrick Aussems alisema anatambua ugumu wa mchezo huo kutokana na rekodi nzuri ya Mazembe wakiwa nyumbani.

Alisema maandalizi ya wiki moja waliyofanya yanamuaminisha kuwa tayari kuwapa changamoto Mazembe.

"Hatuiogopi Mazembe bali tunaiheshimu, tunajua mchezo utakuwa mgumu kwa maandalizi ya nje ya uwanja lakini sisi tutapambana uwanjani," alisema.

Nahodha John Bocco, alisema wanaenda wakiwa na imani kubwa ya kusonga mbele katika hatua ya nusu fainali.

"Kiujumla wachezaji wote tupo vizuri kuelekea mchezo huu, tunaenda kupambana na kuhakikisha tunaibuka na ushindi na kusonga mbele," alisema Bocco.