Dk Mengi: kila mchezaji Serengeti Boys kulamba Sh20milioni wakifuzu Kombe la Dunia

Muktasari:

Serengeti Boys itaanza kutupa karata yake ya kwanza kwenye Fainali za Afcon kwa kucheza na Nigeria Jumapili katika mchezo utakaoanza saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa

Dar es Salaam. Mlezi wa timu ya Vijana ya Serengeti Boys, Dk Reginald Mengi ameahidi kutoa Sh20 Milioni  kwa kila mchezaji endapo watashinda mechi mbili katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon U-17) zitakazowawezesha kufuzu Fainali za Kombe la Dunia Brazil.

Serengeti Boys itaanza kutupa karata yake ya kwanza kwenye Fainali za Afcon kwa kucheza na Nigeria Jumapili katika mchezo utakaoanza saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa.

 Mengi alitoa ahadi leo kupitia kwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla ya Utoaji wa vyeti vya sifa kwa askari mbalimbali wanaofanya vizuri zaidi,iliyofanyika kwenye uwanja wa kituo cha Polisi Oysterbay.

Pia, Mengi ameahidi Sh10 milioni kwa chombo cha habari kitakachoripoti mara kwa mara matukio ya mechi hizo huku akipanga kumpa mhamasishaji bora Sh2 milioni.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Paul Makonda amesema hakujua kama walevi wana nguvu katika kuhamasisha watu.

Makonda amesema ameyabaini hayo kwa namna walivyojitokeza kuhamasisha mechi kati ya Taifa Stars dhidi ya Uganda, ambayo Stars ilishinda kwa mabao 3-0 na kufuzu Afcon.

Mkuu huyo wa mkoa aliwaomba watu kujitokeza kwa wingi uwanjani kuishangilia Serengeti Boys kama walivyofanya kwa Taifa Stars.

 "Kwa kweli nimeiona nguvu ya walevi,basi niwaombe msituache katika mechi hizi zinazowakabili Serengeti Boys," alisema Makonda.

Wakati huo huo Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe leo anatarajia kuzindua wimbo maalumu kwa ajili ya Fainali za Afcon.