Nyie! Huyu Kagere anakitaka kiatu cha ufungaji bora Ligi ya Mabingwa

Muktasari:

Kwa sasa katika orodha ya wafungaji Ligi ya Mabingwa, kinara ni straika wa Al-Nasr ya Libya, Moataz Al-Mehdi akiwa na mabao saba, moja zaidi na aliyonayo Kagere wa Simba

Dar es Salaam. Wikiendi hii hatma ya timu nne za kucheza nusu fainali itafahamika wakati mechi nne tofauti zikipigwa barani Afrika ikiwamo wa Simba na TP Mazembe itakayopigwa mjini Lubumbashi, DR Congo, lakini unaambiwa straika Meddie Kagere akili yake yote ipo kwenye Kiatu cha Dhahabu.

Straika huyo wa Simba mwenye mabao sita kwa sasa katika Ligi ya Mabingwa Afrika amesema kiu yake ni kuona timu yake ikivuka nusu fainali, lakini pia ikiwezekana afunge mabao yatakayompa nafasi ya kunyakua tuzo ya Mfungaji Bora Afrika.

Kwa sasa katika orodha ya wafungaji Ligi ya Mabingwa, kinara ni straika wa Al-Nasr ya Libya Moataz Al-Mehdi akiwa na mabao saba, moja zaidi na aliyonayo Mnyarwanda huyo wa Simba ambaye tangu kutua kwake Msimbazi amekuwa msaada mkubwa hata katika Ligi Kuu Bara akiifungia mabao 14.

Kagere kwenye orodha hiyo analingana mabao na Themba Zwane wa Mamelodi Sundowns ambaye naye amefunga mabao sita kisha wakifuatiwa kwa karibu na kiungo fundi ya Simba, Clatous Chama aliyefunga matano.

Kagere, Chama na Zwane wana nafasi ya kuongeza idadi ya mabao wakati timu zao wikiendi hii zitakapokuwa uwanjani kucheza mechi za marudiano za robo fainali, Simba ikivaana na Mazembe baada ya suluhu ya jijini Dar es Salaam na Mamelodi ikirudiana na Al Ahly ya Misri ugenini.

Katika mechi yao ya kwanza ya Mamelodi iliishindilia Al Ahly mabao 5-0 na kuwapa kazi nzito ya kupanda mlima ikitakiwa kushinda mabao 6-0 ili isonge mbele kucheza nusu fainali.

Kagere alisema kwanza anachoangalia ni kuisaidia timu yake kuweza kupata matokeo mazuri katika mechi yao na Mazembe kama malengo yao yalivyo na kupata nafasi ya kusonga mbele katika hatua ya robo fainali.

“Baada ya hapo ndio nitajiangalia, natakiwa kufunga zaidi ili niwe mfungaji bora na si katika Ligi ya Mabingwa bali katika mashindano yote jambo ambalo nina imani kwa timu yangu hilo linawezekana.