Mtihani: Mastaa wa Manchester United kukatwa mishahara

Muktasari:

Manchester United pia inaonekana kupitia kamba nyembamba katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuchapwa 1-0 katika pambano la awali na Barcelona nyumbani kwao Old Trafford juzi Jumatano usiku.

Manchester, England. Asiyefanya kazi na asile. Ndicho ambacho Manchester United imeamua kwa mastaa wake. watakatwa mishahara yao kwa asilimia 25 kama wakishindwa kufuzu kutinga katika michuano ya Ligi ya mabingwa wa Ulaya.

Roho mbaya hii sio ya ghafla ghafla tu. hivi ndivyo ilivyo kwa katika mpangilio wa mishahara ya mastaa wa United kwa mujibu wa mikataba yao. Watalazimika kukatwa robo ya mishahara yao kama wakishindwa kuipeleka timu yao katika michuano ya Ligi ya mabingwa.

Jambo hilo limewatia nguvu Real Madrid katika mbio zao za kumchukua staa wa United, Paul Pogba ambaye wameanza kumnyatia kwa kasi kwa ajili ya kumchukua katika dirisha kubwa lijalo la majira ya joto ambapo wapo tayari kuvunja benki kwa ajili ya staa huyo.

Mchezaji mwingine ambaye United inapambana kumbakisha ni kipa, David de Gea ambaye anataka mshahara mkubwa zaidi ili abaki Old Trafford lakini endapo United itakosa nafasi nne za juu itakuwa na kazi kubwa ya kumuongezea mshahara zaidi staa huyo wakati wao wakiangalia zaidi namna ya kushusha mishahara.

Staa mwingine ambaye anaweza kuathirika na suala hili ni nyota Marcus Rashford ambaye bado hajasaini mkataba mpya lakini anaweza kujikuta akikatwa mshahara wake kama klabu itaangukia katika michuano ya Europa.

Nyota wa kimataifa wa Chile, Alexis Sanchez tayari anatakiwa kuondoka klabuni hapo bila ya kujali kama United itafuzu katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya au vinginevyo. United inataka kuondokana na mshahara wake mkubwa wa Pauni 500,000 kwa wiki ambao unawaumiza.

Mpaka sasa United wanasimama katika nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi kuu England na ipo katika upinzani mkali kutoka kwa Chelsea, Tottenham na Arsenal katika kuwania nafasi mbili za kucheza Ulaya baada ya Manchester City na Liverpool kuonekana kuzitwaa nafasi mbili za awali.

Manchester United pia inaonekana kupitia kamba nyembamba katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuchapwa 1-0 katika pambano la awali na Barcelona nyumbani kwao Old Trafford juzi Jumatano usiku. Wana kazi ngumu wiki ijayo watakaporudiana na Barcelona ugenini.

Ubingwa wa Ulaya ni moja kati ya njia ambayo inaweza kuwarudisha United katika michuano hiyo msimu ujao lakini kwa jinsi hali ilivyo mambo yatakuwa magumu kwao kutokana na kuruhusu kichapo cha nyumbani. 

Kupunguzwa kwa mishahara kwa wachezaji ni kwa ajili ya kuilinda United mapato ya United yasishuke kutokana na klabu hiyo kupoteza pesa nyingi pindi inaposhindwa kushiriki katika michuano ya Ligi ya Mabingwa.

Kama vile haitoshi, baadhi ya kampuni ambazo zinadhamini United itapunguza pesa wanazoingiza klabuni hapo kama United itashindwa kufuzu katika michuano hiyo msimu ujao. Hii ni kwa mujibu wa vipengele vya mikataba baina yao.

Kampuni ya Adidas itapunguza asilimia 30 ya dau ambalo wameweka Manchester United endapo timu hiyo itashindwa kufuzu katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa misimu miwili mfululizo.

United pia itashindwa kuwa na mvuto kwa baadhi ya mastaa ambao inawafukuzia kwa ajili ya kuongeza makali ya kikosi chao msimu ujao. Mastaa wengi ambao inawafukuzia ni wale ambao klabu zao zinashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kama vile, Kalidou Koulibaly wa Napoli, Toby Alderwierld wa Tottenham na kipa, Jan Oblak wa Atletico Madrid