Kagere, Bocco wajazwa upepo kinoma kwa TP Mazembe

Muktasari:

Simba itakuwa ugenini dhidi ya Mazembe waliotoka nao sare isiyo ya mabao katika mechi iliyopita ya riobo fainali ya michuano hiyo ya CAF na kesho inahitaji kupata sare yoyoye ya mabao ama kushinda ili kufikia rekodi yao ya mwaka 1974 ya kucheza nusu fainali ya Afrika.

Mwanza. Wakati Simba ikishuka uwanjani kesho Jumamosi kuvaana na TP Mazembe ya DR Congo katika mechi ya marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, mashabiki wa timu hiyo mkoani hapa wamewajaza upepo nyota wao, wakiamini wakikomaa ugenini watapata ushindi na kufuzu nusu fainali.
Simba itakuwa ugenini dhidi ya Mazembe waliotoka nao sare isiyo ya mabao katika mechi iliyopita ya riobo fainali ya michuano hiyo ya CAF na kesho inahitaji kupata sare yoyoye ya mabao ama kushinda ili kufikia rekodi yao ya mwaka 1974 ya kucheza nusu fainali ya Afrika.
Wakizungumza wakati wa kikao cha Umoja wa Matawi kilichofanyika Igombe jijini hapa, mashabiki hao walisema wana imani na timu yao katika mchezo wa marudiano kushinda na kusonga mbele.
Mwenyekiti wa matawi hayo, Salya Ludanha alisema kutokana na ushirikiano walionao kwa sasa wanaamini Simba itafanya vizuri bila kujali ipo nyumbani au ugenini.
“Pamoja na suluhu ya mechi ya kwanza nyumbani, haijalishi Simba ipo ugenini au wapi sisi tunatarajia timu yetu ifuzu hatua ya nusu fainali, hivyo tunaamini kina Kagere, Bocco na wenzake watafanya mambo, ni wachezaji wanojituma na kutupa raha mashabiki wao,” alisema Ludanha.
Naye Katibu wa matawi hayo, Nassib Naimocha alisema lengo la kikao hicho ilikuwa ni kuimarisha matawi na kuweka mikakati ya mapema ya mapokezi ya Simba pindi itakapokuja Kanda ya Ziwa.
Kwa upande wake Shabiki, Mallaki Walles alisema anavutiwa na mwenendo wa timu hiyo, huku akishauri wachezaji wanapaswa kupambana kadri ya uwezo wao ili kuendelea kuwapa raha.