Manchester United yajisalimisha nguzo Koulibaly, Alderweireld

Manchester, England. Manchester United imepoteza mechi mbili mfululizo kwa mabao ya mabeki wao kujifunga na sasa wameona inatosha baada ya kuweka mezani kwa Napoli mzigo wa Pauni 90 milioni kumnasa beki wa kati wa kiwango cha dunia, Kalidou Koulibaly.
Hakuna namna, Man United inatazamiwa kutumia pesa nyingi sana kwenye dirisha lijalo la usajili kutengeneza timu itakayokuwa na ushindani kwenye Ligi Kuu England msimu ujao baada ya mambo yao kuwa magumu kwa msimu huu wakiteswa kwenye mechi nyingi ikiwamo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya juzi Jumatano usiku wakati beki Luke Shaw alipojifunga na kuwapa Barcelona ushindi muhimu wa ugenini uwanjani Old Trafford.
Sambamba na beki huyo wa kati, staa mwingine anayehusishwa na Man United kwa sasa ni kiungo wa Everton, Idrissa Gueye huku pia kukiwa na mpango wa kumnyakua staa wa Sporting Lisbon, Bruno Fernandes.
Beki Koulibaly amekuwa akihusishwa na mpango wa kutua Old Trafford ndani ya miezi michache ya karibuni na ripoti za kutoka Italia zinafichua kwamba kuna ofa ya Pauni 90 milioni imewekwa mezani kwa ajili ya kumng'oa beki huyo Msenegali huko Napoli akakipige Man United.
Koulibaly mwenye umri wa miaka 27 amecheza mechi zaidi ya 200 kwenye kikosi cha Napoli tangu alipojiunga hapo akitokea Genk mwaka 2014. Man United inamsaka pia beki mwingine, Toby Alderweireld kutoka Tottenham, ambaye wameambia wanaweza kumpata kwa Pauni 25 milioni tu.