Msuva awatia ndimu wachezaji wa Serengeti Boys

Muktasari:

Msuva ni miongoni mwa wachezaji waliokulia katika akademi za soka sasa anatesa na kikosi cha wakubwa maarufu kama Taifa Stars itakayoshiriki fainali za Mataifa ya Afrika nchini Misri.

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Difaa El Jadida ya Morocco, Saimon Msuva amesema wachezaji wa timu ya vijana ya Tanzania yenye umri chini ya miaka 17 wanatakiwa kutumia vema fursa waliyopata ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana (U17).

Msuva mwenye mabao 10 aliyofungwa msimu huu Ligi Kuu Morocco  alisema macho na masikio yake kuanzia Aprili 14 hadi Aprili 28 atayaelekeza nyumbani (Tanzania) katika fainali hizo za pili kushiriki kwa Serengeti Boys.

Msuva alisema fursa waliyonayo vijana hao mbali na kuiletea heshima taifa ni kujitangaza wao wenyewe ili waweze kupata nafasi za kujiunga na klabu kubwa barani Ulaya.

"Wenzetu wa Afrika Magharibi sio ajabu kuna wachezaji wao wanatoka kwenye timu kubwa za vijana Ulaya, tunawezaje na sisi kuwa na wachezaji wetu huko ni kwa kutumia hii fursa.

"Mpira wa sasa ni vijana nimekuwa shuhuda huku Morocco, wanamkazo kwenye soka la vijana, watafuta vipaji wengi kutoka sehemu mbalimbali naamini watakuwa Tanzania.

"Uwepo wao huko ni ngumu kumuacha mchezaji ambaye atawavutia, Tanzania tuna vipaji vya soka kuchelewa kwetu kutoka ndiko kuliko tukwamisha watu kututambua," alisema Msuva.

Aliongeza Msuva: "Kama tungekuwa na wachezaji wengi ambao wanatamba Ulaya nadhani tusingetegemea mashindano kama haya ili vijana wetu waonekane.

"Ukiangalia makubwa ambayo wachezaji wa Ivory Coast, Nigeria na Misri wanayoyafanya Ulaya ni rahisi watafuta vipaji kwenda kwenye mataifa hayo kuchukua vipaji."