Serengeti Boys inakazi, Uganda yawabeba nyota wa Express, Cagliari, URA Afcon U17

Muktasari:

Timu ya taifa ya Uganda yenye umri chini ya miaka 17, imetua nchini ikiwa na wachezaji 21, akiwemo Ssekimbegga na kujichimbia kwenye hoteli ya Peacock iliyopo katikati mwa jiji la Dar es Salaam (Kariakoo).

Dar es Salaam. Nyota wa Express ya Uganda, Kevin Ssekimbegga ni miongoni mwa mastaa waliobeba matumaini ya taifa hilo katika fainali za mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17, zinazotarajiwa kuanza kutimua vumbi Aprili 14-28.

Timu ya taifa ya Uganda chini ya umri wa miaka 17 ipo Kundi A na wenyeji wa fainali hizo, Tanzania ambao watakutana nao Aprili 17 majira ya saa moja usiku, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Ssekimbegga ni beki wa kulia ameripotiwa na vyombo vya habari vya taifa hilo kuwa ni miongoni mwa wachezaji wenye uzoefu wa kutoka kwenye kikosi chao.

Uganda wameweka kambi kwenye hoteli ya Peacock na kuwa wanafanya mazoezi kwenye uwanja wa GymKhana uliopo Posta, wametua nchini na wachezaji 21.

Orodha kamili ya wachezaji hao ni makipa: Oyo Delton (Kirinya Jinja SS FC), Jack Komakech (Ndejje University FC), and Mubiru Patrick (Bright Stars FC).

Nyota wengine: Kevin Ssekimbegga (Express FC), Ibrahim Juma (KCCA FC), Kasozi Samson (Bright Stars FC), Kizito Mugweri Gavin (Vipers SC), Opira Innocent (Ndejje University), Ssekajja Davis (Bright Stars FC), Kakaire Thomas (Bright Stars FC), Iddi Abdul Wahid (Cagliari FC – Italia).

Mwaka Polycarp (Ndejje University FC), Opaala Edrine Mukisa (Kirinya Jinja SS FC), John Kokas Alou (URA FC), Jarieko James (Paidha Black Angels FC), Asaba Ivan (Vipers SC), Najib Yiga (Vipers SC), Mugulusi Isma (Kirinya Jinja SS FC), Mugisha Rogers (Mbarara City FC), Opiro Justine (KCCA SA), Kawooya Andrew (Vipers SC)