VIDEO: Viwanja AFCON U17 Bongo ni hatari ‘fire’

Muktasari:

Mechi za mashindano hayo zitachezwa kwenye viwanja viwili ambavyo ni ule wa Taifa pamoja na Azam Complex ambavyo vyote viko jijini Dar es Salaam, huku mazoezi kwa timu hizo yakipangwa kufanyika kwenye  viwanja vya Azam Complex, Uhuru, Jakaya Kikwete Youth Park, Gymkhana na HOPAC.

Dar es Salaam.Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 (AFCON U17) zinaanza Jumapili hii jijini Dar es Salaam zikishirikisha mataifa nane yanayowania ubingwa na nafasi nne za kufuzu kwa Kombe la Dunia U17 Oktoba mwaka huu nchini Brazil.
Tayari timu za Morocco, Cameroon na wenyeji Tanzania 'Serengeti Boys' zipo nchini tangu mwanzoni mwa wiki hii huku timu za Uganda na Senegal zikitegemewa kuwasili jana na nyingine zilizobaki zikiwasili leo na kesho.
Mechi za mashindano hayo zitachezwa kwenye viwanja viwili ambavyo ni ule wa Taifa pamoja na Azam Complex ambavyo vyote viko jijini Dar es Salaam, huku mazoezi kwa timu hizo yakipangwa kufanyika kwenye  viwanja vya Azam Complex, Uhuru, Jakaya Kikwete Youth Park, Gymkhana na HOPAC.
Mtandao wa Mwanaspoti.co.tz unakuletea dondoo kuhusu viwanja vitakavyotumiwa na timu kwa ajili ya mechi na mazoezi kwa timu zinazoshiriki AFCON U17.


Uwanja wa Taifa
Kufunguliwa: Mwaka 2007
Mmiliki: Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Eneo Chang'ombe, Dar es Salaam
Nyasi: Asili
Mashabiki: 60,000
Matumizi: Mechi 10 (Makundi mechi 6, nusu-fainali 2, mshindi wa tatu na fainali)
Kauli ya meneja - Nsajigwa Gordon
"Uwanja uko tayari kutumika kwa mashindano. Hakukuwa na marekebisho makubwa kwa sababu tayari uwanja wetu ulikuwa unatumika kwa mechi za kimataifa na ulikuwa unakidhi vigezo husika.


Marekebisho machache yaliyofanyika ni kuboresha vyumba vya kubadilishia nguo vile ambavyo vilikuwa havitumiki hivyo sasa vitatumika vinne badala ya viwili na pia vyumba vya waamuzi sasa vitakuwa vinne. Kuziweka nyasi za uwanja katika ubora. Masuala ya umeme tumejiandaa vilivyo na kila ambacho tumeelekezwa na Shirikisho la Mpira Afrika (CAF) tumekifanyia kazi. Kikubwa ni kuwaomba tu mashabiki watakaokuja uwanjani pamoja na timu kutunza miundombinu ya uwanja na yeyote atakayeharibu, tutamchukulia hatua kali za kisheria," alisema Nsajigwa

Azam Complex

Mmiliki: Azam Football Club
Eneo: Chamazi, Dar es Salaam
Kufunguliwa: Mwaka 2013
Nyasi: Bandia
Mashabiki: 10,000
Matumizi: Mechi 6 (Makundi)


Kauli ya Meneja - Sikitu Kilakala
"Sisi kama Azam tuna furaha kubwa kwa uwanja wetu kupitishwa na CAF utumike kwa mechi za fainali hizi za Mataifa ya Afrika kwa vijana. Maandalizi kwa upande wetu yamekamilika kwa 98% na hiyo iliyobaki haizuii uwanja kutumika.
Mambo ambayo tulikuwa tukiyafanyia kazi ni marekebisho ya eneo la kukaa waandishi wa habari na ukumbi wao wa mikutano, eneo wanalokaa wageni rasmi, maboresho ya mfumo wa usalama, tiba, tiketi na utoaji taka lakini pia vyumba vya kubadilishia nguo na waamuzi ambavyo vimeongezeka.


Gharama zote za ukarabati ambazo zinazidi Shilingi 400 milioni zimetolewa na Azam ikiwa ni mchango wake katika kusaidia kufanikisha mashindano haya," alisema Bi. Kilakala

Jakaya Kikwete Youth Park

Mmiliki: Symbion
Eneo: Kidongo Chekundu, Dar es Salaam.
Kufunguliwa: 2015
Nyasi: Bandia
Matumizi: Mazoezi
Ofisa: Bahati Mgunda


"Tunaamini uwepo wa mashindano haya ni fursa nzuri ya kuibua ari ya michezo kwa nchi. Kituo chetu kina furaha kubwa kupewa nafasi ya kutumika kwa ajili ya mazoezi ya timu. Miundombinu yetu iko vizuri kwa sababu hadhi ya kituo na uwanja wetu ni ya kimataifa. Ukaguzi umekamilika na vile viti tulivyoambiwa tuvifanyie kazi tumeshafanya hivyo.

Kimsingi kila kitu kipo tayari na kiuhalisia kitendo cha timu kufanya mazoezi hapa kitasaidia kuhamasisha watoto wadogo ambao wanautumia uwanja huu bure," alisema Mgunda.



Uwanja wa Uhuru

Mmiliki: Serikali
Eneo: Chang'ombe, Dar es Salaam
Nyasi: Bandia
Kufunguliwa: Mwaka 1961
Matumizi: Mazoezi
Meneja: Nsajigwa Gordon

"Uwanja wa Uhuru utatumika kwa mazoezi hivyo nao haukuwa na marekebisho makubwa zaidi ya yale ya kuondoa kapeti la nyasi za zamani na kuweka mpya na zoezi hilo kimeshakamilika," alisema Gordon.


Viwanja vingine
Viwanja vingine ambavyo vitatumika ni vile vya Gymkhana na HOPAC ambavyo vinamilikiwa na watu binafsi. Viwanja hivyo vitatumika kwa ajili ya mazoezi ya timu.
Viwanja: Gymkhana & HOPAC
Wamiliki: Watu Binafsi
Nyasi: Asili
Matumizi: Mazoezi.