Usicheke, hii ngoma Manchester United, Barcelona bado mbichiiiii!

Thursday April 11 2019

 

Manchester, England. SIR Alex Ferguson amesema yake kuhusu namna ya kumdhibiti Lionel Messi. Rio Ferdinand naye amesema yake akiwaambia wachezaji wa Manchester United wanavyopaswa kumkabili supastaa huyo wa Barcelona waliyekabiliana naye usiku wa jana Jumatano na kufungwa bao 1-0.
Lakini, kilichotokea kimetokea na hakuna kitu cha kucheka sana, kwa sababu kuna mechi za marudiano na kwenye soka la Ligi ya Mabingwa Ulaya, maajabu yamekuwa ni mambo ya kawaida tu. Huko kwenye Uwanja wa Old Trafford kulikuwa mshikemshike, wakati mastaa moto kabisa kama Romelu Lukaku, Paul Pogba, Marcus Rashford, Anthony Martial na Jesse Lingard walipojaribu kuonyesha dunia kile wanachoweza kukifanya walipomkabili Messi na jeshi lake la Barcelona kwenye mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu. Maajabu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hakuna asiyeyafahamu. Man United kwenye raundi iliyopita waliwaduwaza PSG, timu ambayo Barcelona pia waliwahi kufanya maajabu yao, licha ya wapo wakikumbuka kwamba AS Roma waliwafanya vibaya msimu uliopita tu hapo.
Mechi nyingine matata iliyopangwa kufanyika kwa usiku wa jana, Ajax walikuwa kwao Amsterdam kumkaribisha Cristiano Ronaldo na jeshi lake la Juventus, kilichotokea kimetokea, lakini bado vita haijakwisha, kuna kipute kingine kitapigwa Turin wiki ijayo. Juzi Jumanne, Tottenham Hotspur waliwakaribisha Manchester City kwenye uwanja wao mpya na Hueng-min Son alimaliza mechi kwa kufunga bao pekee kwenye mechi hiyo kumfanya kocha Mauricio Pochettino kumfuata Pep Guardiola kwenye mechi ya marudiano huko Etihad akiwa na faida ya ushindi kwenye mechi ya kwanza japo ni mwembamba. Liverpool waliposhuka kwenye uwanja wao wa Anfield kuwakaribisha FC Porto, walivuna matokeo bomba mabisa, Mbili Bila, wakiweka wavuni mabao yao kupitia kwa Naby Keita na Roberto Firmino. Lakini, kocha wa Liverpool anafahamu wazi desturi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ilivyo, suala la kupindua matokeo halijawahi kuwa gumu na ndio maana amewaambia wachezaji wake kujiandaa kisaikolojia wakati watakapokwenda Ureno kwenye mechi ya marudiano, watarajia kushambuliwa mwanzo mwisho na wapinzani wao FC Porto.
"Mbili Bila ni matokeo mazuri sana, niliyatarajia kabla ya mechi na ndio yaliyopatikana. Lakini, yote kwa yote, hii ni mbili bila na mechi bado inaendelea. Hivyo tunapaswa kupambana. Bila shaka, Porto watajaribu kufanya kila kitu kwenye mechi ya marudiano na hakika itakuwa mechi ngumu sana," alisema Klopp.
Kocha wa Man United, Ole Gunnar Solskjaer amekuwa akidai kwamba kwa yale matokeo yaliyoyapata dhidi ya PSG yanawafanya kuwa na imani kwamba wanaweza kufanya maajabu kwenye ligi hiyo ya msimu huu na kusonga mbele mdogo mdogo hadi fainali.
Kwa mechi zilizopigwa juzi na jana ni mwanzo tu wa mapambano na kwamba vita bado inaendelea hatima ya kila timu itafahamika baada ya michezo ya maruduano itakayopigwa wiki ijayo. Fainali ya mwaka huu ya michuano hiyo ya Ulaya itapigwa kwenye uwanja wa Atletico Madrid huko Hispania.

Advertisement