Kesi ya Wambura upelelezi bado, yapigwa kalenda hadi Aprili 25

Muktasari:

Katika mashtaka hayo 17; shtaka moja ni la kughushi, shtaka moja la kutoa na kuwasilisha nyaraka za uongo; mashtaka 13 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na mashtaka mawili ya kutakatisha fedha haramu.

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili, aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa wanapitia nyaraka muhimu kabla ya kukamilisha upelelezi.

Wambura akikabiliwa na mashtaka 17 yakiwemo ya kutakatisha fedha zaidi ya Sh 100milioni, katika kesi ya uhujumu uchumi namba 10/2019.

Wakili wa Serikali, Batilda Mushi ameieleza Mahakama hiyo, leo April 11, 2019, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Mushi, amedai mbele ya Hakimu Mfawidhi, Kelvin Mhina, kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kwa sasa wapitia nyaraka muhimu ambazo hawawezi kuziweka wazi.

"Upelelezi wa shauri hili bado haujakamilika na upande wa mashtaka bado tu tunaendelea kupitia nyaraka muhimu, hatuwezi kuzisema ni nyaraka zipi, ila  upande wa utetezi wajue tu kwamba kuna nyaraka muhimu tunazifanyia kazi kabla ya kukamilisha upelelezi wa kesi hii," alidai Mushi.

Mushi baada ya kueleza hayo, Wakili wa mshtakiwa, Majura Magafu aliutaka upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi kwa wakati.

Hakimu Mhina baada ya kusikiliza maelezo ya pande, aliutaka upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi kwa wakati ili kesi hiyo iweze kusonga mbele.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi April 25, 2019 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na mashtaka ya utakatishaji fedha yanayomkabili kutokuwa na dhamana.

Kwa mara ya kwanza, Wambura alifikishwa Kisutu, Februari 11, 2019, akikabiliwa na mashtaka 17 yakiwemo ya kutakatisha fedha zaidi ya Sh 100milioni.

Katika mashtaka hayo 17; shtaka moja ni la kughushi, shtaka moja la kutoa na kuwasilisha nyaraka za uongo; mashtaka 13 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na mashtaka mawili ya kutakatisha fedha haramu.

Katika shtaka la kwanza ambalo ni la kughushi, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 6, 2004, sehemu isiyojulikana ndani ya jiji la Dar es Salaam.

Siku hiyo, Wambura kwa nia ya kutapeli  alitengeneza barua ya  kughushi ambayo haina kumbu kumbu namba akionyesha  imeandikwa na E Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa  kampuni ya Jeck system anadai kurejeshewa malipo ya mkopo wa USD 30,000 pamoja na riba aliyokuwa ameikopesha TFF.

Katika shtaka la kutoa na kuwasilisha nyaraka ya uongo, mshtakiwa  alitoa barua iliyokuwa haina kumbu kumbu namba  ya Julai 6, 2004, akijifanya kwamba ni barua iliyoandikwa na E. Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Jeck System Ltd, akionyesha kuwa anadai mkopo wa USD 30,000 pamoja na riba waliokopeshwa TFF huku akijua kuwa siyo kweli.

Hata hivyo, kuanzia shtaka la tatu hadi la 15 mshtakiwa anadaiwa kujipatia kiasi cha zaidi Sh 95 milioni, kwa njia ya udanganyifu akidai kuwa fedha hizo ni sehemu ya malipo ya jumla ya kiasi cha fedha mbali mbali na riba kutoka kwa kampuni ya Jeck System Ltd huku akijua kuwa siyo kweli.

Pia katika mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, Wambura anadiawa kutenda kosa hilo, Juni 17, 2015 huko katika ofisi za TFF, ambapo kwa njia ya udanganyifu, mshtakiwa alijipayia Sh 10milioni kutoka TFF kwa kuonesha kuwa ni malipo ya USD 30,000 pamoja na riba kutoka kwenye kampuni hiyo ha Jeck jambo ambalo siyo kweli.

Katika shtaka la utakatishaji fedha, Wambura anadai, kati ya Agosti 15 na Oktoba 21, 2014, makao makuu ya Shirikisho hilo, alijipatia Sh 25milioni kutoka TFF huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la kughushi.

Pia, shtaka jingine utakatishaji fedha haramu, Mshtakiwa anadaiwa kati ya Machi 16 na Oktoba 21 2015, alijipatia Sh 75,947,924 kutoka TFF wakati akijua fedha hizo siyo halali na zimetokana na shtaka la kughushi.