Prisons, Lipuli, Biashara United zagawa dozi nzito Ligi Kuu

Muktasari:

Mabao ya Prisons katika mchezo huo yalifungwa na Salumu Kimenya dakika ya 35 na Adam Adam dakika ya 45.

Dar es Salaam. Prisons imeendelea kutakata katika Ligi Kuu Bara baada ya leo Jumatano kuifunga Mwadui mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Tangu timu hiyo inolewa na kocha Mohammed Adolph Rishard imekuwa na kiwango bora huku ikishinda mechi zote sita ilizocheza kwenye Uwanja wake wa nyumbani tangu mwaka huu uanze.

Mabao ya Prisons katika mchezo huo yalifungwa na Salumu Kimenya dakika ya 35 na Adam Adam dakika ya 45.

Kwenye Uwanja wa Samora Iringa wenyeji Lipuli wameichapa African Lyon mabao 2-0. Mabao ya washindi yamefungwa na Zawadi Mauya dakika ya 60 na Miraji Athumani dakika ya 90.

Uwanja wa Mabatini Mlandizi Ruvu Shooting imelazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar.

Mtibwa Sugar ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya saba kupitia kwa Riphat Hamis kabla ya Fulluzulu Maganga kuisawazishia Ruvu Shooting dakika ya 23.

Kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida,wenyeji  Singida Unitd wameifunga Alliance Fc mabao 2-0. Mabao ya Singida United yamefungwa na Kennedy Juma dakika ya 29 na Frank Zakaria dakika ya 45.

CCM Kirumba Mwanza, wenyeji Mbao wamelala kwa bao 1-0 dhidi ya Biashara United. Bao la washindi limefungwa na George Maganga dakika ya 45 wakati kwenye Uwanja wa  Mkwakani Tanga, Coastal Union imetumia vema uwanja wake wa nyumbani kwa kuifunga Stand United bao 1-0 lililofungwa dakika ya 63 na Raizin Hafidhi.