Safari ya wanariadha mbio za dunia yaiva

Muktasari:

Msafara wa timu hiyo ya Tanzania unaundwa na watu 20, wachezaji 16 na viongozi wanne.

Dar es Salaam. Safari ya kikosi cha wanariadha wa Timu ya Taifa kushiriki mbio za dunia za nyika imeiva.
Timu hiyo itaagwa Kesho Machi 27 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe tayari kwa safari ya kwenda mjini Aarhs Denmark kwenye mashindano hayo yatakayofanyika Machi 30.
Wanariadha 28 walikuwa kambini kujiandaa na mbio hizo kwa ufadhili wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), na DStv imewasilia Dar es Salaam Leo Machi 26 tayari kwa safari.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday alisema amesema vijana wana ari ya kwenda kupeperusha vema Bendera ya Taifa huko Denmark.
Gidabuday, amesema Waziri Mwakyembe, ataongoza hafla ya kuipa Baraka za mwisho timu hiyo ikiwamo kukabidhi Bendera ya Taifa, akiungana na viongozi mbalimbali kuanzia saa 8 mchana kwenye ukumbi wa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika hafla hiyo pia wamemualika Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Ngorongoro, Mkurugenzi wa Multchoice Tanzania na Kurugenzi za Michezo Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Msafara wa timu hiyo ya Tanzania unaundwa na watu 20, wachezaji 16 na viongozi wanne.
Amewataja viongozi hao ni Makamu wa Pili wa Rais- Ufundi RT, Dk. Hamad Ndee ambaye ni Mkuu wa Msafara, Kocha Mkuu Meta Petro, Kocha Msaidizi Madai Jambau na Matron Marcelina Gwandu.
Wachezaji kwa upande wa wanaume ni Marko Monko, Joseph Panga ‘Mti Mkavu’, Faraja Damas, Emmanuel Giniki, Gabriel Geay, Francis Damiano na Yohana Elisante.
Wanawake ni Failuna Matanga, Magdalena Shauri, Angelina Tsere, Sisilia Ginoka, Mayselina Mbua, Amina Mgoo, Anastazia Dolomongo, Aisha Magelani na Natalia Elisante.
Timu hiyo itaondoka usiku wa Machi 27 kwa ndege ya KLM na inatarajiwa kurejea nchini Machi 31