VIDEO: Watanzania mzuka umepanda waingia uwanjani mapema kuiona Taifa Stars, Uganda

Muktasari:

Uganda tayari imefuzu kwa fainali hizo na kuiacha vita ya kupata timu moja ya kuungana naye kwa nchi tatu Tanzania, Lesotho na Cape Verde.

Dar es Salaam. Watanzania wameanza kujitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kushuhudia mechi ya Tanzania dhidi ya Uganda wa kusaka kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika 2019, Misri.

Mchezo huo unatarajia kupigwa saa kumi na mbili jioni (12:00), lakini muitikio wa mashabiki umekuwa mkubwa.

Mwanaspoti online ilishuhudia idadi kubwa ya mashabiki hao wakianza kuingia uwanjani kuanzia saa 7:00 mchana kiasi cha kuanza kutoa taswira ya uwanja huo kujaa mapema.

Ni saa sita tu zimesalia kuelekea mpira huo kuanza, lakini idadi ambayo imejitokeza inadhihirisha kwamba baadae kutakuwa hapatoshi ndani ya uwanja wa Taifa.

Mashabiki wakimiminika uwanjani kushuhdia mchezo huo ambao mgeni rasmi atakuwa waziri mkuu, Kassim Majaliwa.

Baadhi ya mashabiki walisema wamefika kwenye uwanja wa Taifa saa 3 Asubuhi wakisubiri mchezo wa saa 12 jioni.

"Nilikuwa natamani siku ifike, hivyo jana sijalala, nilipoamka cha kwanza ilikuwa ni safari ya uwanjani," alisema Mtanzania, Kassim Haidary.

Mtanzania mwingine, Jackosn Patrick alisema amefika uwanjani Asubuhi, sababu hakutaka kusimuliwa chochote kuhusu mchezo huo.

"Milango ilipofunguliwa tu nilikuwa uwanjani, sioni tabu kukaa hata masaa 12 kusubiri mchezo kama huu wa timu yangu ya taifa," alisema.

Hadi saa nane mchana baadhi ya majukwaa ya mzunguko wa Orange upande wanaokaa mashabiki wa Yanga yalikuwa yamejaa.

ULINZI USIPIME

Katika upande wa ulinzi katika mechi hii umeonyesha kuwa mkubwa baada ya Polis kuzunguka mara kwa mara wakiangalia namna ambavyo watanzania (mashabiki) wanavyopata nafasi ya kuingia uwanjani.

Polisi wakizunguka kila kona iliyokuwa karibu na uwanja kuhakikisha utulivu na amani ukiwa wa hali ya juu.

Kila mtu ashinde kwao

Kila mtu ashinde kwao ndiyo kauli mbiu Watanzania leo wanapaswa kuiomba kila mtu ashinde kwao. Tanzania ifunge Uganda na Cape Verde iwachapa Lesotho.

Mechi za mwisho zitaamua hatma ya Tanzania na Lesotho zenye pointi tano kila moja na Cape Verde ikiwa na pointi nne ili kuungana na Uganda yenye pointi 13.

Hata hivyo, muhimu ni Stars kwanza washinde ndipo wachungulie kwingine.

Uganda, Tanzania, Lesotho na Cape Verde, zipo kundi L. Msimamo ni kuwa Uganda wanaongoza kwa pointi 13, Lesotho ya pili ina pointi 5, Tanzania ya tatu na pointi 5, wakati Cape Verde ipo namba nne na pointi zake nne.

Uchambuzi ni kuwa Uganda imeshafuzu, maana imecheza mechi 5, imeshinda nne na kutoka sare moja. Nafasi kwenye kundi inawaniwa na timu zote tatu zilizobaki. Kila timu, kwa maana ya Tanzania, Lesotho na Cape Verde, inaweza kupata tiketi ya kwenda Afcon leo.

Tukianza na Cape Verde inayoshika mkia. Ikishinda leo dhidi ya Lesotho, itafikisha pointi 7. Endapo Stars itapigwa na Uganda, maana yake wao ndiyo watamaliza wa pili kwenye msimamo nyuma ya Uganda. Vilevile Uganda na Stars wakitoka suluhu au sare, bado Cape Verde wakiifunga Lesotho watakwenda Afcon, kwani Stars itafikisha pointi 6, wakati Cape Verde watakuwa na 7.

Lesotho ina pointi sawa na Stars. Kwa leo, ndiyo timu ambayo inapaswa kupigana ili ishinde na moja kwa moja itafuzu Afcon hata kama Stars itaifunga Uganda kwa ushindi wowote ule. Lesotho wanabebwa na kanuni za Caf za uendeshaji wa michuano ya Afcon.

Kwa mujibu wa ibara ya 14 ya Kanuni za Afcon (Regulations of the Africa Cup of Nations), timu zinapolingana pointi (Tiebreakers), kinachotazamwa ni sheria ya head-to-head, yaani katika timu mbili zilizolingana, zilipokutana, nani alipata nini dhidi ya mwenzake?

Kama timu zimepata pointi sawa, yaani katika mechi mbili, kila timu ikapata pointi 3, kinachofuata ni kutazama ni nani kapata magoli mengi walipokutana. Kisha yupi anakuwa na kashinda magoli mengi ugenini. Kama kote watakuwa wamelingana ndiyo inatazamwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa kwenye kundi zima. Mwisho ndiyo bahati nasibu kama kote wamelingana asilimia 100.

Kanuni zinasema Stars akishinda na Lesotho akampiga Cape Verde, moja kwa moja Lesotho anakwenda Afcon. Maana wote watafikisha pointi 8, halafu kanuni ya kwanza kutazamwa ni ibara ya 14.1.1, inayosema aliyepata pointi nyingi katika mechi zilizokutanisha timu mbili zinazolingana pointi, ndiye anakwenda.

Katika pointi 5 za Lesotho, 4 imezipata kutoka Stars. Ilitoka sare ya 1-1 na Stars Chamazi Complex, kisha ikaifunga Stars 1-0 kwenye Uwanja wa Setsoto, jijini Maseru. Hivyo kikanuni, Lesotho wakishinda leo, moja kwa moja wanakwenda Afcon.

Kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa, Stars ipo mbele ya Lesotho. Stars in hasi 2, Lesotho ni hasi 4. Hata hivyo, tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa ipo ibara ya 14.1.5. Yaani ni kipengele cha tano kutazamwa. Ni mbali mno.