Ni zamu yetu

JAMANI hawa mbona wanakufa tu, nyie tulieni mnachotakiwa kukifanya uwanjani ni kushangilia kwa nguvu kubwa. Inafahamika kuwa Watanzania hivi sasa hawana kitu kingine wanachosubiri zaidi ya ushindi katika mchezo wao dhidi ya Uganda, ambao ni wa kufuzu Fainali za AFCON kule Misri, baadaye mwaka huu.

Stars anahitaji ushindi ili isonge mbele kama itafikisha pointi nane zitakazowafanya wakae nafasi ya pili wakitanguliwa na Uganda ambao, tayari wamefuzu huku wakiomba matokeo mabaya kwa Lesotho ambao watakuwa uwanjani kukipiga na Cape Verde.

Kocha Mkuu wa Stars, Emmanuel Amunike anafahamu kiu ya Watanzania na kuamua kufanyia kazi kubwa safu yake ya ushambuliaji baada ya kubaini kuwa na mapungufu.

Katika mazoezi ya jana Jumamosi asubuhi, Amunike alipangia kazi maalum washambuliaji wake akiwataka kutumia kila nafasi wanayoipata wanapokuwa kweye eneo la wapinzani.

Mazoezi ambayo alikuwa anazingatia kuhakikisha wanafunga kila aina ya mpira, baada ya kuwapa zoezi la kupiga mipira ya adhabu ndogo huku shughuli nzima ikikjabidhiwa kwa Simon Msuva na Mbwana Samatta.

Pia, alikuwa akiwataka mabeki wake wanapocheza faulo wawe na umakini katika kutengeneza ukuta huku akiwaonya kuacha kurukaruka wote kwa pamoja bila maelewano na kipa.

Upande wa kona alikuwa akiwatumia zaidi Shiza Kichuya na Gadiel Michael kupiga kona ambazo zitaingia moja kwa moja ndani ya 18 na sio kutoka, zoezi ambalo lilinoga kwani mastraika walikuwa na kazi moja tu ya kupasia mpira nyavuni.

MANULA, YONDANI MH

Wakati mazoezi hayo yanaendelea Kelvin Yondani alishindwa kufanya mazoezi baada ya kukaa nje huku akifungwa barafu mguu wa kulia kiasi cha kuzua hofu kwa mashabiki waliokuwa wamejitokeza uwanjani.

Mwanaspoti lilipomuuliza Daktari wa Taifa Stars, Richard Yomba ambaye alisema Yondani alishindwa kufanya mazoezi baada ya kupata mshtuko katika mguu.

“Hajaumia, alikuwa anapata mpozo si unajua kacheza mechi nyingi, yupo vizuri nilimpumzisha kwa muda tu,” alisema.

Akizungumzia ishu ya Aishi Manula kushindwa kufanya mazoezi ya asubuhi uwanja wa Boko Veterani, alisema kipa huyo alikuwa na ruhusa kwenda hospitalini.

“Manula hayupo kwa sababu ameenda hospitali kufanyiwa matibabu ya mkono, alishtua mkono wake lakini tuna imani kubwa Jumapili (leo) atakuwepo,” alisema.

MSUVA AONGEZA MZUKA

Msuva, ambaye anaichezea Difaa El Jadida ya Morocco, amewatoa hofu wapenzi wa soka nchini kwa kusema lazima watawatoa kimasomaso kwenye mchezo huo.

Alisema kama atapata nafasi ya kuanza kwenye mchezo huo, atajitahidi kushirikiana vema na wenzake ili kupata matokeo mazuri. “Kila mchezaji anatambua umuhimu wa huo mchezo, tumekuwa na maandalizi mazuri ambayo yalijikita kwenye mbinu za namna ya kuwafunga wapinzani wetu.

“Tuna kila sababu ya kuweka historia kwenye ardhi yetu ya nyumbani, imetosha kuwa watazamaji wa wenzetu ambao miaka nenda miaka rudi wamekuwa wakishiriki michuano hiyo,” alisema Msuva na kuongeza: “Hii ni zamu yetu naamini itakuwa hivyo, inatakiwa tujivunie kuwa Watanzania, uzalendo utatubeba. Unaweza usiwe na jezi ya Taifa Stars lakini ukivaa nguo yenye rangi ya taifa itapendeza zaidi.”

Ushindi wa Taifa Stars dhidi ya Uganda na kufungwa kwa Lesotho au sare mbele ya Cape Verde kutaifanya Tanzania kuingia kwa mara ya pili kwenye Fainali za Afcon.

Mara ya kwanza kwa Taifa Stars kushiriki Afcon ilikuwa miaka 39 iliyopita nchini Nigeria ambako iliishia katika hatua ya makundi.