Wawa akabidhiwa watatu Mazembe

SIMBA kwasasa imejificha kwenye kivuli cha Taifa Stars lakini kuanzia kesho Jumatatu akili yao itaanza kufikiria mchezo wa Robo Fainali dhidi ya TP Mazembe na ili wafanikiwe mchongo wao mzima utatoka hapa.

TP Mazembe inayoongoza ligi ya nchini kwao DR Congo wakiwa na pointi 60 Simba ili washinde safu yao ya ulinzi chini ya Pascal Wawa na Erasto Nyoni inatakiwa kujiapiza kutokubali kuwaachia mastraika wao watatu.

Mastraika hao ni Jackson Muleka anayevaa jezi namba 17, mkongwe Tresor Mputu na Elia Meschack ambao ndiyo roho ya ushindi ya timu hiyo yenye makombe matatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mastraika hao wote watatu wamekuwa na kasi kubwa katika kufumania nyavu kila mmoja akiwa na mabao matatu na kama Wekundu hao wakiwabana hawa tu mambo yatakuwa rahisi.

Habari nzuri kwa Simba ni kwamba katika mchezo baina ya timu hiyo wanaoanzia nyumbani ambako hajawahi kutoka yeyote Mazembe huanza na mastraika hao wawili tu huku mmoja akianzia benchi.

Lengo lao ni kuwa na ulinzi mkubwa na katika mfumo wao wa 3-5-2 wakiwa ugenini umekuwa ukiifanya safu yao ya ulinzi kupitika kirahisi endapo ikipewa presha kubwa katika mashambulizi ya kushtukiza.

Msimu huu ambao Mazembe imepoteza mechi moja pekee katika Ligi ya Mabingwa walipochukua 3-0 ugenini dhidi ya Constantine ya Tunisia huku pia ikitoa sare mbili ugenini.

Mfumo huo umekuwa ukipigiwa kelele nchini kwao ambapo pia kocha wa timu hiyo Mihayo Pamphile aliurudia tena alipocheza ugenini dhidi ya AS Vita Club na akakubali kipigo kingine cha mabao 3-0.

Nyumbani kazi ipo

Wanapokuwa nyumbani Simba italazimika kujiandaa vizuri ambapo wanakuwa na mfumo tofauti wakianza na mastraika hao watatu mbele na kuwa na kasi ya hatari.

Njia kubwa ya mashambulizi ya Mazembe ni kutumia mabeki wao wa pembeni na hata viungo wao washambuliaji ndiyo wanakuwa injini ya ushindi.

Ndugu yake Okwi tishio

Mmoja ya watu hatari katika safu ya kiungo ya Mazembe sasa ni Mganda Joseph Ochaya anayetumia mguu wa kushoto huku mgongoni akiwa na jezi namba 6.

Ochaya amekuwa na krosi za hatari ambazo zimekuwa chakula kizuri kwa Muleka,Mputu na hata beki Mondeko Zatu ambaye naye amefikisha mabao matatu msimu huu akipanda na kushuka.

Simba haitatakiwa kufanya makosa karibu na lango lao ambapo bahati mbaya kwa Ochaya katika mipira yake ya adhabu ni mipira kugonga besela lakini ikirudi uwanjani tayari kuna watu wanasubiri watupie wavuni.