Sikia Bale anachosema kuhusu staa Ronaldo

Muktasari:

Bale alijiunga na Real Madrid akitokea Tottenham Hotspur kwa ada iliyoweka rekodi ya dunia kipindi hicho mwaka 2013 alipotua Bernebau kwa Pauni 85 milioni.

SUPASTAA wa Real Madrid, Gareth Bale amefunguka na kusema hajawahi kuwa na bifu lolote na Cristiano Ronaldo kwa muda wote waliokuwa pamoja Santiago Bernabeu.

Mastaa hao mara kadhaa wameripotiwa kutokuwa na uhusiano mzuri katika kipindi ambacho Ronaldo alikuwa kwenye kikosi cha Los Blancos kabla ya kutimkia Juventus mwaka jana.

Bale amekuwa na wakati mbaya tangu Mreno huyo alipoondoka huku wengi wakiamini angepaswa kuwa kwenye kipindi kizuri kwa sababu yule aliyekuwa akimsumbua ameshaondoka Bernabeu.

“Cristiano ni mchezaji wa ina yake, muda wote nilifurahia kucheza naye,” alisema Bale.

“Shida ni kwamba vyombo vya habari vilijaribu kukuza jambo ambalo halijawahi kuwapo. Sisi tulikuwa vizuri tu. Ni mchezaji wa aina yake alichokifanya kwenye timu hasa kwenye kufunga mabao ni jambo kubwa. Ni mchezaji mkubwa na hivyo ndivyo alivyo hadi sasa.”

Bale alijiunga na Real Madrid akitokea Tottenham Hotspur kwa ada iliyoweka rekodi ya dunia kipindi hicho mwaka 2013 alipotua Bernebau kwa Pauni 85 milioni.