Mourinho bana, eti kazikataa ofa kibao

Muktasari:

Mourinho aliyejipachika mwenyewe jina la The Special One, alifutwa kazi Desemba mwaka jana huko Man United baada ya kushinda mechi mbili tu kati ya nane za mwisho na kibarua chake kilifika kikomo kufuatia kichapo cha 3-1 kutoka kwa mahasimu wao, Liverpool

London,England. Jose Mourinho ameibuka na kudai ameshakataa ofa za kazi tatu au nne hivi kwa anajua anachokitaka kabla ya kurudi kwenye kazi yake ya ukocha.
Bosi huyo wa zamani wa Manchester United na Chelsea alisema anatumia pia muda huu ambao hayupo kibaruani baada ya kufutwa kazi huko Old Trafford kupumzika kabla ya kurudi akiwa fiti kwelikweli kuwashika wapinzani wake.
Mourinho aliyejipachika mwenyewe jina la The Special One, alifutwa kazi Desemba mwaka jana huko Man United baada ya kushinda mechi mbili tu kati ya nane za mwisho na kibarua chake kilifika kikomo kufuatia kichapo cha 3-1 kutoka kwa mahasimu wao, Liverpool. Licha ya kuboronga huko Old Trafford ofa mbalimbali za kazi bado zinatumwa kwa Mreno huyo ambaye mwenyewe amesema anasubiri kazi sahihi anayoitaka.
"Ni miezi mitatu na nusu sana tangu nilipoachishwa kazi na nipo kwenye maandalizi nikisubiri kazi mpya. Unapokuwa kocha, unakosa muda wa kupumzika, hivyo natumia kipindi hiki kupumzika," alisema.
"Kazi ya ukocha ni spesho na naifurahia sana kazi hiyo. Nataka kurudi mwishoni mwa msimu huu, kuanzia Juni ili nianze msimu vyema. Nafahamu nisichokitaka na ndio maana nimekataa ofa tatu au nne hivi. Najua ninachokitaka na naamini nitakipata."
Mourinho amekuwa akihusishwa na Inter Milan pia, ambayo aliwahi kuinoa huko nyuma na kubeba mataji matatu makubwa mwaka 2010. Alihusishwa na Real Madrid, lakini wababe hao wa Bernabeu wameamua kumrudisha Zinedine Zidane kundini baada ya kumtimua Santiago Solari wiki iliyopita.