Pogba,Griezmann ni vuta nikuvute

Muktasari:

Kilichopo ni kwamba kuna orodha kubwa sana ya mastaa wanaotajwa mwishoni mwa msimu huu watatoka England kwenda Hispania, lakini wapo wengine watakaotoka upande huo na kuhamia huku kwenye ligi ya makocha moto kabisa akiwamo Pep Guardiola

London,England. Maisha yanakwenda kasi sana. La Liga kwa sasa ina timu moja tu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakati Ligi Kuu England imeingiza timu nne kwenye hatua ya robo fainali ya michuano hiyo msimu huu.
Hilo linatajwa ni mabadiliko ya ubora kwenye michuano hiyo ya Ulaya.
Lakini unaambiwa hivi jambo hilo litaleta mtifuano mkubwa kwenye dirisha lijalo la usajili kwani kutakuwa na vuta nikuvute ya klabu za Ligi Kuu England na zile za La Liga kwenye kunyang'ana mastaa. Kilichopo ni kwamba kuna orodha kubwa sana ya mastaa wanaotajwa mwishoni mwa msimu huu watatoka England kwenda Hispania, lakini wapo wengine watakaotoka upande huo na kuhamia huku kwenye ligi ya makocha moto kabisa akiwamo Pep Guardiola.
Ligi Kuu England imetajwa kuwa bora zaidi kwa sasa kwanza kutokana na kuvutia makocha wa maana.
Makocha wote moto Ulaya kwa sasa wapo kwenye ligi hiyo na kwamba ni miezi michache tu imepita tangu Jose Mourinho alipofutwa kazi, lakini kinyume cha hapo, basi makocha wote bora unaowafahamu wewe wapo kwenye ligi hiyo.
Jambo hilo litaleta vita kubwa, La Liga hawatakubali wanataka kurudisha makali yao na ndio maana kuna mastaa kibao kwenye Ligi Kuu England wanahusishwa na mpango wa kuhamia huko Hispania kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Huko Real Madrid kinachoripotiwa ni kwamba wanataka kuwapa Liverpool ofa ya beki Raphael Varane ili wao wamchukue straika Sadio Mane.
Hiyo ina maana dili hilo likifanikiwa, basi Varane atatua England na Mane atakwenda Hispania.
Lakini Los Blancos wana orodha nyingine ndefu ya wachezaji inaowasaka, akiwamo staa wa Chelsea, Eden Hazard, kiungo wa Tottenham, Christian Eriksen, kiungo wa Manchester United, Paul Pogba na fowadi wa Old Trafford, Marcus Rashford. Lakini Mane anasakwa pia na Barcelona.
Orodha hiyo ya mastaa inamhusu pia kipa David De Gea ambaye imedaiwa huenda Madrid wakaamua kumrudisha Thibaut Courtois kwenye Ligi Kuu England ili wao wamchukue kipa huyo Mhispaniola namba moja wa huko Man United.
Kiungo wa Chelsea, N'Golo Kante naye yupo kwenye orodha. Wakati hilo la kuwahusisha mastaa wengi wa Ligi Kuu England wakitajwa kwamba wanaweza kutimkia Hispania mwishoni mwa msimu huu, vigogo wa England nao hawataki mchezo na kuhusishwa na mastaa kibao wa kutoka kwa La Liga, ikiwamo Isco, Toni Kroos kutoka Madrid, huku Philippe Coutinho na hata Ivan Rakitic wakitoka kwenye kikosi cha Barcelona huku taarifa hizo zikimhusu pia supastaa wa Atletico Madrid, Antoine Griezmann anayesakwa huko Manchester kwa nguvu zote.
 
Kwa upepo ulivyo kwa sasa, La Liga imepania kurudi kwenye makali yake na ndio maana inalenga kuchota mastaa tupu wa kutoka England ambapo kwenye msako wao yupo pia fowadi wa Manchester City, Raheem Sterling.
Mastaa wa Spurs, Harry Kane na Dele Alli hawatajwi kwa sasa, lakini chochote kinaweza kutokea kwenye dirisha lijalo la usajili.
La Liga inaingia kwenye vita kali na Ligi Kuu England hata kwenye mchakato wa kuwanasa mastaa wa Paris Saint-Germain, Neymar na Kylian Mbappe.
Hivi ndivyo inavyoelezwa vita itakayokuwa mwishoni mwa msimu huu baina ya La Liga na Ligi Kuu England katika kutafuta ubabe wa soka la Ulaya.