Bilionea shabiki wa Man United anavyotaka kuinunua Chelsea

Muktasari:

Ratcliffe mwenye umri wa miaka 66 alizaliwa huko Failsworth, Lancashire, nje kidogo ya jiji la Manchester na makuzi yake yote amekuwa akiishabikia Manchester United.

London,England. Mtu tajiri zaidi Uingereza yote anataka kuinunua klabu ya soka la Chelsea.
Tajiri huyo anaitwa Sir Jim Ratcliffe, bilionea mwenye pesa zake. Kinachoelezwa ni kwamba bilionea huyo anamiliki utajiri wa Pauni 21 bilioni.
Ratcliffe mwenye umri wa miaka 66 alizaliwa huko Failsworth, Lancashire, nje kidogo ya jiji la Manchester na makuzi yake yote amekuwa akiishabikia Manchester United.
Na sasa bilionea Ratcliffe anataka kuinunua Chelsea kutoka kwenye umiliki wa bilionea wa Kirusi, Roman Abramovich. Kama Ratcliffe atafanikiwa kuinunua Chelsea, basi atakuwa mmiliki wa timu ya soka tajiri zaidi duniani. Baada ya miaka 15 ya kuwa chini ya Abramovich, Chelsea sasa inaweza kuwa chini ya umiliki wa mtu tajiri zaidi kwenye soka.
Orodha ya Matajiri iliyotolewa na gazeti la Sunday Times, ilimtaja Sir Jim Ratcliffe, kuwa mtu tajiri zaidi Uingereza yote. Bilionea huyo makazi yake yapo Manchester.
Kama Sir Jim Ratcliffe atachukua timu ya Chelsea, vita itakuwa kwenye orodha ya matajiri zaidi wanaomiliki timu za soka England na Ulaya kwa ujumla.
Hii hapa orodha ya wamiliki matajiri zaidi wa klabu za soka duniani ambao watapaswa kujipanga kutokana na ujio wa Ratcliffe kwenye mchezo huyo kama atafanikiwa kumvua Abramovich kikosi cha Chelsea chenye maskani yake huko Stamford Bridge. Miongoni mwa matajiri hao wamiliki wa klabu za soka duniani, watano wanamiliki klabu za Ligi Kuu England, lakini utashangaa bilionea wa Manchester City, Sheikh Mansour, siyo namba moja. Matajiri hao ni hawa hapa.

9. Joe Lewis - Tottenham, Pauni 3.8 bilioni
Tottenham Hotspur kwa madirisha mawili mfululizo wameshindwa kufanya usajili, lakini si kwamba hawana pesa ya kufanya hivyo, mmiliki wao ana pesa ndefu balaa. Mmiliki wa klabu hiyo, Joe Lewis, ni moja ya watu matajiri waliopo Uingereza, ambaye ameripotiwa kutoa Pauni 800 milioni kusaidia ujenzi wa uwanja mpya wa Tottenham. Bilionea huyo anatajwa kuwa na utajiri wa Pauni 3.8 bilioni.

8. Zhan Jindang - Inter Milan, Pauni 5.2 bilioni
Bilionea wa Kichina mwenye pesa nyingi kupitia biashara zake mbalimbali, Zhan Jindang aliichukua Inter Milan mwaka 2016. Tangu alipotua kwenye timu hiyo walau mambo yamebadilika na Inter sasa imekuwa ikipata mafanikio ya ndani ya uwanja. Inter walibadilika kutoka kwenye nafasi ya saba 2017 na kumaliza ligi wakiwa nafasi ya nne na hivyo kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2018.

7. Shahid Khan - Fulham, Pauni 5.4 bilioni
Baada ya kushuhudia timu yake ikishuka daraja katika msimu ambao aliinunua, Shahid Khan ametoa mkwanja mrefu kuhakikisha kikosi hicho kinarudi kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Bilionea huyo amekuwa si mwoga pia wa kufanya uamuzi baada ya kumfuta kazi kocha Slavisa Jokanovic na kumleta Claudio Ranieri kabla ya kumwondoa Mtaliano huyo na kumpa kazi Scott Parker kama kocha wa muda. Bilionea huyo ametumia zaidi ya Pauni 100 milioni kusajili wachezaji 12 wapya mwaka jana.

6. Stan Kroenke - Arsenal, Pauni 6.4 bilioni
Anafahamika kwa jina la ‘Silent Stan’ huko Arsenal. Bilionea Stan Kroenke utajiri wake aliokuwa nao hauendani kabisa na bajeti ya usajili ya kocha Unai Emery kwenye kikosi hicho cha Emirates. Kocha Emery amekuwa na bajeti ndogo sana ya usajili kiasi cha kulazimika kunasa wachezaji kwa mkopo kama alivyofanya kwa Denis Suarez kwenye dirisha la Januari. Bosi huyo, Kroenke ana timu nyingine pia anazomiliki, lakini ishu yake huko Arsenal amekuwa mgumu wa kutumia pesa nyingi kwenye usajili.

5. Roman Abramovich - Chelsea, Pauni 8.3 bilioni
Ndiye mtu aliyeibadili Chelsea kutoka kuwa timu ya kawaida kwenye Ligi Kuu England na kuwa moja ya klabu kubwa kabisa Ulaya. Bilionea huyo wa Kirusi, Roman Abramovich aliinunua Chelsea Juni 2003. Hadi kufikia mwaka 2006, Chelsea ilikuwa imebeba mataji ya Ligi Kuu England mfululizo, ikiwa ni mawili zaidi ya ambayo walibeba kabla ya Abramovich hajachukua timu. Kwa mashabiki wa Chelsea, bilionea Abramovich amewaonyesha kwamba inawezekana kununua furaha.

4. Philip Anschutz - LA Galaxy, Pauni 10 bilioni
Amepewa tuzo ya heshima huko Marekani kutokana na mchango wake mkubwa anaotoa kwenye soka. Bilionea Philip Anschutz ni mmiliki wa klabu ya LA Galaxy inayoshiriki Ligi Kuu Marekani. Kwenye kikosi hicho amefanya mambo makubwa ikiwamo kuwasajili David Beckham, Steven Gerrard na Zlatan Ibrahimovic kuifanya timu hiyo kuwa kubwa zaidi kwenye soka la Marekani na ndiyo maana wameshinda taji la Ligi Kuu England mara kibao.

3. Andrea Agnelli - Juventus, Pauni 10.4 bilioni
Rais wa Juventus, Andrea Agnelli na familia yake ndiyo wamiliki wa klabu hiyo matata kabisa kwenye Serie A. Kwa kuimiliki klabu hiyo tangu mwaka 1947, familia ya Agnelli ndiyo inayoripotiwa kumiliki timu ya mpira kwa miaka mingi zaidi huko Italia. Licha ya kuwa na pesa nyingi, Juventus wamekuwa si watu wa kutumia sana pesa kwenye kufanya usajili na ndiyo maana wachezaji wake wengi inawanasa kwa uhamisho wa bure kama ilivyotokea kwa mastaa kibao akiwamo Andrea Pirlo, Dani Alves, Paul Pogba na Aaron Ramsey.

2. Sheikh Mansour - Man City, Pauni 17 bilioni
Baada ya kushuhudia mahasimu wao Manchester United wakitamba kwenye soka kwa muda mrefu, Manchester City wakaleta mwekezaji na tangu timu ilipoanza kuwa chini ya umiliki wa Sheikh Mansour, wamekuwa moto ndani ya uwanja. Miamba hao wamebeba mataji matatu ya Ligi Kuu England ndani ya kipindi cha karibuni na kuonyesha kwamba umiliki wa bilionea huyo kuwa na maana kwenye timu hiyo. Mansour na kampuni zake zimekuwa na umiliki wa timu nyingine kama vile ya New York City FC, ambayo imefanya usajili wa mastaa wa maana kama vile David Villa, Andrea Pirlo na Frank Lampard.

1. Dietrich Mateschitz - New York Red Bulls, Pauni 17.8 bilioni
Mwanzilishi mwenza wa kampuni ya kinywaji cha Red Bull, Mateschitz amekuwa akihusishwa kwa namna kubwa sana kwenye michezo, ikiwamo umiliki wake wa klabu ya New York Red Bulls. Timu hiyo imekuwa na nguvu kubwa ndani ya uwanja tangu ilipokuwa chini ya bilionea huyo kutokana na uwekezaji wake na matumizi ya pesa anayofanya kwenye timu hiyo. Kwa mabilionea hawa waliopo kwenye timu, yule anayetaka kuinunua Chelsea mwenye utajiri wa Pauni 21 bilioni, atakuwa kiboko yao zaidi.