Nyota hawa waitesa Gor Mahia

Muktasari:

Straika hatari na tegemeo Mrwanda Jacques Tuyisenge, winga Boniface Omondi na kipa Fredrick Odhiambo nao hawatakuwepo kwenye mechi hiyo ya raundi ya kwanza ya mchujo wa nane bora

JAPO Gor Mahia imefuzu hatua ya nane bora kwenye dimba la CAF Confederation Cup baada ya kumaliza ya pili kwenye kundi D, kocha wake angali ana mtihani mkubwa kuendelea mbele.
Hii ni kwa sababu Oktay atawakosa wachezaji watano nyota kwenye mechi ya raundi ya kwanza na wapinzani wajao kwenye hatua hiyo ya nane bora.
Wachezaji hao tegemeo kwenye kikosi cha kwanza cha Gor, wote  atawakosa kutokana na kadi walizolishwa kwenye mechi za hatua ya makundi.
Kiungo mhimili, Ernest Wendo na beki wa kushoto Mganda, Shafik Batambuze wataikosa raundi ya kwanza ya mechi hiyo kutokana na kadi nyekundu walizolishwa Jumapili  kwenye ushindi wao wa 1-0 dhidi ya Petro Atletico wa Angola.
Straika hatari na tegemeo Mrwanda Jacques Tuyisenge, winga Boniface Omondi na kipa Fredrick Odhiambo nao hawatakuwepo kwenye mechi hiyo ya raundi ya kwanza ya mchujo wa nane bora, baada ya kulishwa kadi ya pili ya njano dhidi ya hao Atletico.
Kutokana na hali hiyo, kocha Oktay sasa atalazimika kumtegemea straika mkongwe Dennis Oliech ambaye amemtumia sana kama sub kuongoza safu yake ya mashambulizi.
Oliech atasaidiana na Nicholas Kipkurui ambaye amekuwa kwenye fomu ya kutisha toka ajiunge na Gor msimu huu. Mastraika Erisa Ssekisambu na Francis Mustafa ambao hawajaonyesha viwango, nao wakuwa mbadala kwa mipango ya Oktay.
Kwenye nafasi yake Batambuze, kocha Oktay atalazimika kumwita Geoffrey Ochieng kujaliza pengo hilo huku nafasi yake winga Omondi, akimpa fursa George ‘Black Berry’ Odhiambo. Nafasi yake Wendo, kocha Oktay anaye Kenneth Muguna ambaye hajatumika sana huku langoni atalazimika kumpanga chaguo la pili Boniface Olouch.
Kwa wakati huo, kocha Oktay kasema atakuwa akiingia sokoni kwenye dirisha hili dogo la usajili kusaka wachezaji watatu, beki, winga na fowadi mwingine. Kocha Oktay kasema kama akiwapata wachezaji sahihi anaohitaji katika nafasi hizo, basi kikosi chake kitakuwa kamili kado kufanya mambo.