Liverpool yaishusha kileleni Manchester City

Muktasari:

Liverpool inapambana kupata ubingwa wa kwanza msimu huu baada ya kusubiri kwa zaidi ya miaka 30.

London, England. Liverpool imerejea kileleni mwa Ligi Kuu England shukrani kwa penalti ya James Milner iliyowapa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Fulham.

Liverpool ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na  Sadio Mane likiwa ni bao lake la 11 katika mashindano yote hadi sasa, lakini bado wageni hao walishindwa kutumia nafasi ya kupata bao la mapema kuwapoteza wenyeji wao Fulham.

Kukosa mawasiliano mazuri kati ya beki Virgil van Dijk na kipa Alisson kulitoa mwanya kwa Ryan Babel kufunga bao la kusawazisha kwa wenyeji katika dakika 74.

Lakini uzembe wa kipa wa Fulham, Sergio Rico kwa kumvuta bila ya sababu Mane aliyekuwa akiwahi mpira uliopigwa na Mohammed Salah ulisababisha mwamuzi kutoa penalti.

Kiungo Milner hakufanya makossa kwa kufunga penalti hiyo na kuiweka Liverpool kileleni kwa mara ya kwanza tangu Februari.

Vijana wa Jurgen Klopp kwa sasa wapo mbele kwa pointi mbili kwa Manchester City wenye mchezo moja mkononi.