Juventus kiguu na njia kwa Kante

Muktasari:

Ripoti zinadai Juventus ipo kwenye mazungumzo na mawakala wa Kante kwa ajili ya kupata huduma ya kiungo huyo Mfaransa.

Turin, Italia. JUVENTUS kumbe bana iliilegeza Chelsea kwa kuipa kwa mkopo mshambuliaji wake Gonzalo Higuain. Unajua kwanini? Ikiwa imepita miezi kadhaa tangu ilipoipata mshambuliaji huyo, Juventus imepanga kuvamia huko Stamford Bridge kwa lengo la kwenda kumng'oa kiungo mkabaji, N'Golo Kante.
Ripoti zinadai Juventus ipo kwenye mazungumzo na mawakala wa Kante kwa ajili ya kupata huduma ya kiungo huyo Mfaransa.
Tuttosport inadai uongozi wa Juventus unaamini Kante atashawishika kuihama Chelsea kwenye dirisha lijalo la usajili na kwenda kujiunga na timu yao licha ya mapema tu msimu huu kusaini mkataba mpya huko Stamford Bridge ambao utamtaka akae klabuni hapo hadi mwaka 2023.
 Juve ipo kwenye mazungumzo hayo, lakini haitakuwa na wepesi katika kumpata Kante kwa sababu Chelsea yenyewe haipo tayari kumpoteza mchezaji huyo. Ugumu mwingine utatokea kwa Real Madrid na Paris Saint-Germain zinazohitaji pia huduma ya staa huyo wa Ufaransa.