Karia: Simba imeanza Taifa Stars itamalizia kwa kufuzu Afcon

Muktasari:

Taifa Stars inahitaji matokeo ya ushindi kwenye mchezo wake huo dhidi ya Uganda ambao tayari wameshafuzu huku wakiiombea Lesotho kupoteza mbele ya Cape Verde ili kupata tiketi ya kufuzu kwa Afcon

Dar es Salaam.Rais wa shirikisho la soka Tanzania (TFF), Wallace Karia ameibuka baada ya Simba kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kusema rekodi nyingine nchini itaweka Jumapili ijayo na Taifa Stars.

Karia alitoa pongezi zake kwa wachezaji, viongozi na mashabiki wa Simba kwa kazi kubwa ambayo waliifanya kuhakikisha Simba inatinga kwenye hatua hiyo kwa mara nyingine tena.

“Rekodi nyingine tunaenda kuweka Watanzania kwenye uwanja huu huu wa taifa pale ambapo Taifa Stars itakuwa ikiikaribisha Uganda kwenye mchezo wa mwisho wa makundi.

“Tunahitaji kuwa miongoni mwa mataifa yatakayoshiriki Afcon baadae nchini Misri, hilo linawezekana kama vile ambavyo Simba walifanya kwa pamoja basi Watanzania sote yatusapa kuungana.

“Tujitokeze kwa wingi ili tuujaze uwanja huu wa taifa, tuwape nguvu wachezaji wetu,” alisema rais huyo wa TFF.

Taifa Stars inahitaji matokeo ya ushindi kwenye mchezo wake huo dhidi ya Uganda ambao tayari wameshafuzu huku wakiiombea Lesotho kupoteza mbele ya Cape Verde ili kupata tiketi ya kufuzu kwa Afcon.