Janja ya Manula ilipowakata stimu wachezaji wa AS Vita

Muktasari:

Pamoja na kuiongoza Simba kufuzu kwa robo fainali Manula ndiye kipa aliyefungwa mabao mengi zaidi katika Kundi D akiwa amefungwa mabao 13

Dar es Salaam. Ni kama walikuwa wanasubiri filimbi ya mwisho ya mwamuzi kutoka Morocco, ili kushangilia ushindi wao.

Ilikuwa hivi. Baada ya Simba kufunga bao la pili na kuonyeshwa dakika zilizosalia, kipa wa Simba, Aishi Manula alijilaza chini kama kawaida yake akidai kubanwa na misuli nyuma ya paja.

Baada ya kujilaza, wakati huo mpira ulikuwa wa faulo, Zana Coulibally alikuwa anatakiwa kupiga faulo hiyo, lakini alisita na kumwonyesha mwamuzi kuwa kipa yuko chini.

Kuona vile Coulibally aliupiga mpira nje, mbali kabisa na mwamuzi akamfuata Manula na pale akatoa kadi huku akiita huduma ya kwanza.

Mwamuzi aliita huduma ya kwanza na wenyewe wakaingia taratibu hadi kwa manula naye alionyesha kuwa ameumia kweli na kujilaza zaidi huku wachezaji wa timu zote wakiwa kwenye mafungumafungu.

Baada ya kumaliza kutibiwa, Manula alifungwa bandeji kwenye paja, lakini mwamuzi hakumwacha salama. Alimtandika kadi ya njano kwa kuchelewesha muda.

Kitendo kile kilipomalizika, alikwenda kuruhusu mpira kurushwa. Simba waliutoa kwa kuwa Manula alikuwa ameumia, lakini AS Vita hawakutaka biashara ya fair play, walirushiana na soka ikaendelea.

Wachezaji wa Simba kuona mbona hawapasiwi, wakaanza kufuatilia kwa nguvu, na ulipofika katikati ya uwanja, filimbi ya kuashiria mpira kumalizika ikapulizwa. Hapo sasa shughuli ikaanza. wachezaji wakapagawa na kushangilia huku mashabiki nao wakiwa wamepagawa.

Baada ya filimbi ile, wachezaji wa AS Vita walilala uwanjani, wengine wakijiinamia ni kama wanasema, Dah! Tumeshamalizwa hapa.