VIDEO: Simba pekee imefuzu kwa pointi chache

Muktasari:

Katika mashindano hiyo, Ismaily ya Misri ndiyo iliyofanya vibaya zaidi kwa kupoteza mechi nne na kumaliza ikiwa na pointi mbili baada ya mechi sita sawa na FC Platnum ya Zimbabwe.

Dar es Salaam. Hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika imemalizika kwa miamba nane kufahamika wakiwemo mabingwa wa Tanzania, Simba.

Simba ambayo imeshinda nyumbani kwake mechi zote, imefuzu baada ya kufikisha pointi tisa ambazo zilivukwa na Al Ahly ya Misri Pekee ambayo ndiyo iliyoongoza katika Kundi D.

Miamba hiyo ya Tanzania ndiyo timu pekee katika michuano hiyo iliyovuna pointi tisa, hakuna timu nyingine kati ya zilizoshiriki iliyopata pointi hizo.

Al Ahly imemaliza ikiwa na pointi 10 wakati JS Saoura ambayo ilikaa kileleni mwa msimamo kwa wiki moja, ilimaliza ya tatu baada ya kupigwa mabao 3-0 na Al Ahly mchezo wa mwisho.

AS Vita ya DR Congo iliyoingia fainali ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita, ilimaliza ikiwa mkiani na pointi zake saba.

Hata hivyo, kati ya timu zilizofuzu, Simba ndiyo timu iliyovuka ikiwa na pointi chache, chini ya 10.

Esperance ya Tunisia kutoka Kundi B iliongoza ikiwa na pointi 14, ikiwa ni pointi nyingi zaidi ya timu yoyote ikifuatiwa na TP Mazembe ambayo ilimaliza ikiwa na pointi 11. TP Mazembe iko Kundi C.

Timu sita zimemaliza michuano hiyo zikikusanya pointi 10 na kufuzu ukiondoa Club Africaine ambayo ilipata pointi 10 lakini imekosa wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa kwa CS Costantine.

Zilizopata pointi 10 kila mmoja ni Wydad Casablanca (Morocco) na Mamelod Sundows ya Afrika Kusini (Kundi A), Horoya (Guinea, Kundi B) na CS Costantine na Club Africain kutoka Kundi C. Al Ahly ni kutoka Kundi D.

Katika michuano hiyo, Ismaily ya Misri ndiyo iliyofanya vibaya zaidi kwa kupoteza mechi nne na kumaliza ikiwa na pointi mbili baada ya mechi sita sawa na FC Platnum ya Zimbabwe.