VIDEO: Sahau kuhusu Chama huyo Bocco, Wawa, Mzamiru usipime kabisa

Muktasari:

Kuingia kwa Simba katika hatua ya Robo fainali inakuwa ni mara ya pili timu hiyo baada ya kufanya hivyo 2003.

Dar es Salaam. Klabu ya Simba imetengeneza rekodi ya kufuzu kwa mara ya pili kwa hatua ya robo fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mabao ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Clatous Chama yalihakikishia Simba kutinga katika hatua hiyo na kuwaacha vichwa chini wachezaji wa AS Vita.

Katika mchezo huo Simba ilionyesha nidhamu ya mchezo baada ya kuwaheshimu wapinzani wao katika kuhakikisha hawafunguki wakiwa nyumbani.

Hata hivyo, Vita ilipata goli la kuongoza dakika 13 kupitia kwa Kazadi Kasengu na kuwanyong’onyesha, lakini hata hivyo walitulia na kujipanga upya.

SAFU YA ULINZI

Katika eneo la ulinzi Pascal Wawa alimtuliza Mundele Makusu ambaye katika mchezo wao wa kwanza uliopigwa nchini Congo alikuwa mwiba baada ya kutupia mabao mawili.

Alichokuwa anakifanya Wawa ni kutembea hatua kwa hatua na Makusu, kitu hiko kilimfanya ashindwe kabisa kuchezea mpira kama ambavyo amezoeleka.

Kocha wa Vita, Ibenge ilimlazimu kumtoa lakini baada ya kufanya hivyo ndio aliwaruhusu Simba watoke nyuma na kuanza kusogea mbele kwa kushambulia haraka.

KIUNGO USIPIME

Eneo la katikati walianza James Kotei, Mzamiru Yassin na Clatous Chama. Ndani ya dakika 15 za mwanzo walionekana kama kupotea lakini baada ya damu kuchanganya walijikuta wakianza kuelewana vya kutosha.

Mzamiru Yassin na James Kotei waliweza kuhakikisha wanakaba vilivyo katika eneo hilo, kiasi cha Luamba Ngoma kupotea katika eneo hilo na Simba kutawala.

Mabadiliko ya kuingia Haruna Niyonzima na Hassan Dilunga yaliweza kuongeza spidi ya kushambulia, huku Niyonzima akiubadilisha mchezo baada ya kila anapokuwa anagusa mpira alikuwa anafosi kusogea juu na kuwafanya Vita wapoteane.

BOCCO USIPIME

Unaweza usimtaje kutokana na kazi yake kujificha lakini ukweli katika mchezo wa jana alikuwa kama injini baada ya kuzunguka muda wote kuhakikisha eneo la ushambuliaji lao halipoi.

Bocco aliwafanya Emmanuel Okwi na Meddie Kagere wawe huru katika mchezo huo baada ya yeye kuzunguka eneo kubwa akihangaika kuhakikisha mabeki wa Vita hawatambi.

Kagere kila alipokuwa anajipanga kutaka kupata bao alikuwa anakutana na kuotea lakini hata hivyo, hakuweza kutupia huku Emmanuel Okwi kila alipokuwa anahangaika kuweka wavuni hakufanikiwa.