Nyie mnamsikia Guardiola huko

Muktasari:

Chama hilo la Guardiola linachuana pia kwenye Ligi Kuu England huku wakiwa kwenye nane bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Manchester, England. Pep Guardiola amekiri kwamba ni lazima abebe taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya ili ahesabike kuwa mtu aliyepata mafanikio makubwa kwenye kikosi cha Manchester City.

Kocha huyo Mhispaniola bado hajaifikisha Man City kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini msimu huu kikosi chake kinapewa nafasi kubwa ya kubeba ubingwa.

Baada ya kupangwa kuwakabili Tottenham kwenye hatua ya robo fainali, Guardiola alisema: “Nilipokuwa Bayern hatukufika fainali na watu walinihukumu kwa hilo.

"Vigezo vyangu ni vya juu sana na ni lazima nivifikie. Nilihukumiwa Munich kipindi kile, hivyo nitachukuliwa kwa jambo hilo leo pia. Ni lazima nikubaliane na hilo.”

Msimu huu Man City wapo kwenye mchakamchaka wa kubeba mataji mane, wakiwa tayari wameshanyakua Kombe la Ligi, jana Jumamosi wamefuzu kwa nusu fainali ya Kombe la FA baada ya kuichapa Swansea mabao 3-2 katika mchezo wa robo fainali.

Chama hilo la Guardiola linachuana pia kwenye Ligi Kuu England huku wakiwa kwenye nane bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

“Kama hatutashinda Ligi ya Mabingwa Ulaya, kazi yetu ya misimu mitatuy itakuwa haina maana,” alisema Guardiola.