Manchester United wachekelea gundu la Messi Ulaya

Muktasari:

Messi alipiga mbili, lakini mashabiki wa Man United wala hamwogopi yeye wala timu yake hasa kutokana na rekodi yao kwenye michuano hiyo inapofikia hatua ya robo fainali

Manchester, England. Manchester United inashughuli pevu mbele ya Barcelona kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini mashabiki wake wanaishi kwa matumaini na kuamini kupenya inawezekana!

Chini ya Ole Gunnar Solskjaer kikosi hicho kimefanya mambo makubwa sana hadi kufikia kwenye hatua hiyo ya robo fainali jambo ambalo lisingekuwa jepesi wangeendelea kuwa chini ya Jose Mourinho, aliyefutwa kazi Desemba mwaka jana.

Lakini, sasa Man United watakabiliwa kuwasukuma nje Barcelona, ambao kwa sasa ndio wanaopewa nafasi kubwa ya kuwa mabingwa baada ya watemi Real Madrid kutupwa nje. Makali ya Messi ndiyo yaliyoifikisha Barca hatua ya robo fainali na msimu huu atakuwa moto uwanjani kusaka medali yake ya tano ya ubingwa wa michuano hiyo.

Kwenye mechi iliyopita, Messi alipiga mbili, lakini mashabiki wa Man United wala hamwogopi yeye wala timu yake hasa kutokana na rekodi yao kwenye michuano hiyo inapofikia hatua ya robo fainali.

Barca wametupwa nje kwenye misimu yote mitatu iliyopita, lakini ikiwa ni mara yao ya nne katika misimu mitano ya karibuni. AS Roma waliwatupa nje msimu uliopita licha ya kwamba mechi ya kwanza walifungwa 4-1, lakini Juventus na Atletico Madrid nazo ziliwafungashia virago.

Lakini, Messi naye amekuwa na wakati mgumu sana inapofika hatua hiyo kwenye michuano ya Ulaya. Messi alicheza mechi 11 za robo fainali bila ya kufunga. Bao lake la mwisho kufunga kwenye hatua hiyo ilikuwa Aprili 2013 kwenye sare ya 2-2 dhidi ya PSG. Hilo ndilo gundu linalomsumbua Messi linalowapa jeuri Man United wakiamini watapenya mbele ya Barcelona.

Mechi za robo fainali ambazo Messi hakufunga bao

2017/18 - Barcelona 4-1 Roma, Roma 3-0 Barcelona

2016/17 - Juventus 3-0 Barcelona, Barcelona 0-0 Juventus

2015/16 - Barcelona 2-1 Atletico, Atletico 2-0 Barcelona

2014/15 - PSG 1-3 Barcelona, Barcelona 2-0 PSG

2013/14 - Barcelona 1-1 Atletico, Atletico 1-0 Barcelona

2012/13 - Barcelona 1-1 PSG (mechi ya pili).