Salah, Mane washika hatma Liverpool kwa Bayern

Muktasari:

Liverpool wanahitaji kushinda katika mchezo huo ili kufuzu kwa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa

Munich, Ujerumani. Liverpool imewafuata mabingwa wa Ujerumani, Bayern Munich kwa lengo moja tu kuhakikisha wanashinda na kusonga mbele kwa hatua ya 16 ya Ligi ya Mabingwa.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa wiki tatu zilizopitia timu hizo zilitoka suluhu kwenye Uwanja wa Anfield, lakini tumaini kubwa la Liverpool lipo kwa washambuliaji wake watatu Mohamed Salah, Roberto Firmino na Sadio Mane endapo watarudi katika ubora wao wa kuzifumania nyavu katika mashindano hayo ya Ulaya.

Tottenham ilikuwa timu ya kwanza ya England kuwatoa Wajerumani baada ya kuichakaza Borussia Dortmund kwa jumla ya mabao 4-0, huku Manchester City ikiwa katika nafasi nzuri ya kusonga mbele baada ya kuichapa Schalke kwa mabao 3-2 katika mchezo wa kwanza.

Hata hivyo, Bayern inayoaminika kuwa ndiyo timu iliyobeba nyota wote wa Ujerumani watakuwa na kazi moja tu ya dhidi ya kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp anayerejea nyumbani.

Baada ya kushindwa kutumia vizuri uwanja wake wa nyumbani wiki tatu zilizopita, hiyo inamaanisha Liverpool lazima wasahau rekodi mbovu ya kutokushinda ugenini kama wanataka kusonga mbele kwa robo fainali.

Msimu uliopita Salah, Firmino na Mane kila moja alifunga mabao 10, katika Ligi ya Mabingwa na kuisaidia Liverpool kufuzu kucheza fainali.

Katika michezo saba waliyocheza msimu huu watatu hao wamefanikiwa kufunga mabao sita tu, manne yakiwa katika mchezo wao wa nyumbani dhidi ya Red Star Belgrade.

Habari mbaya zaidi ni Liverpool imefanikiwa kufunga bao moja tu ugenini katika mechi zake za hatua ya makundi dhidi ya Napoli, Red Star na Paris Saint-Germain na goli hilo pekee lilifungwa kwa penalti na James Milner jijini Paris.

Mane na Firmino wametesti mitambo yao kabla ya safari ya Munich baada ya kila mmoja kufunga mabao mawili katika ushindi 4-2 dhidi ya Burnley Jumapili iliyopita na kuifanya Liverpool kubaki katika nafasi ya pili ikiwa nyuma kwa pointi moja kwa vinara Man City.