Magori afunguka ishu ya Okwi Simba ipo hivi

Muktasari:

Mshambuliaji Emmanuel Okwi alijiondoa dakika ya mwisho katika kikosi cha Simba kilichokuwa kinakwenda Algeria.

Dar es Salaam.Baada ya mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi kukosekana katika kikosi kilichokwenda Algeria, ilianza kuibuka minong'ono kuwa nyota huyo alijiondoa makusudi katika kikosi hicho ili aweze kutulia na kucheza mchezo wa kufuzu Afcon wa Uganda dhidi ya Tanzania.

Mwanaspoti lilidokezwa mchezaji huyo alizima simu yake na kuwaacha njia panda viongozi wa klabu hiyo, lakini baadae aliibuka hotelini na kumuambia kocha wake anaumwa.

Akizungumza baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege Dar es Salaam, Mkurugenzi mtendaji mkuu wa Simba, Crensentius Magori alisema taarifa alizonazo mchezaji wao alikuwa anaumwa na walimuacha nchini baada ya mwalimu kumruhusu abaki.

"Kweli alikuwa hapatikani katika simu na saa chache kabla timu haijasafiri alikuja kuongea na mwalimu na kumwambia hajisikii vizuri hivyo hawezi kucheza mchezo huo, sisi tulipomuuliza alisema alikuwa yupo kwa daktari ndio maana alikuwa hapatikani," alisema.

Akizungumzia kuhusu ishu ya mchezaji huyo kwenda nchini Uganda baada ya timu kuondoka alisema taarifa hizo atazifuatilia kwa umakini ili aweze kujua kama ni kweli au la.

"Ndio kwanza nimetua kwahiyo inabidi nifuatilie kuona kama ni kweli ameenda Uganda, siamini kama ameenda kwa sababu muda bado wa yeye kwenda hata kama ameitwa katika timu ya Taifa, ninachojua mimi Okwi alikuwa anaumwa na alisema muda mchache kabla timu haijasafiri" alisema.

Aliongeza mchezaji huyo atakuwepo katika kikosi chao kitakachocheza dhidi ya AS Vita Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa.