Mingange apewa mikoba ya Pluijm Azam

Muktasari:

Kabla ya kujiunga na kikosi cha vijana cha Azam FC, Meja Mstaafu Abdul Mingange alizinoa Ndanda FC, Mshikamano FC na Mbeya City

Dar es Salaam.Uongozi wa Azam FC, umemtangaza Kocha wa kikosi chao cha vijana, Meja Mstaafu Abdul Mingange kurithi wa nafasi iliyoachwa wazi na Hans Pluijm aliyetimuliwa jana.

Pluijm na kocha wake msaidizi, Juma Mwambusi walitimuliwa na timu hiyo kutokana na mwendelezo wa matokeo yasiyoridhisha ambayo imekuwa ikiyapata kwenye Ligi Kuu katika siku za hivi karibuni.

Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffary Iddi amesema Mingange ataiongoza na kuisimamia timu kwa muda wakati uongozi ukiwa katika harakati za kusaka kocha mpya.

"Sasa rasmi benchi la ufundi kwa kipindi hiki litashikwa na Meja Abdul Mingange na Kocha msaidizi atakuwa ni Iddi Cheche. Awa makocha ni wazoefu ndani ya Azam FC na hii siyo mara ya kwanza kushika timu katika kipindi hiki uongozi unapofanya harakati za kusaka kocha mpya.

“Niweke wazi tu kuwa Iddi Cheche atabakia kuwa kocha msaidizi hata kwa huyo kocha mpya atakayekuja. Ikumbukwe kuwa Pluijm alikuja na kocha wake msaidizi ambaye ni Mwambusi lakini sasa hivi kocha mpya atakuja mwenyewe tu na msaidizi atakuwa ni Cheche," alisema Iddi.

Kwa mujibu wa Iddi, majukumu ya Meja Mingange na Cheche yataanzia kwenye mechi ya Kombe la Azam Sports Federation Cup dhidi ya Rhino Rangers kesho.