Jose Mara, Papii Kocha, Mulemule wanogesha shoo ya Bogoss

Sunday February 24 2019

 

By RHOBI CHACHA

Dar es Salaam. Usiku wa kuamkia leo Jumapili, wanamuziki Jose Mara, Papii Kocha, Mulemule na Jimmy Manzaka walipanda jukwaa la Bogoss Musica kwa nyakati tofauti na kupagawisha mashabiki kwenye Ukumbi wa T Garden uliopo Sinza Kijiweni, Dar es Salaam.

Ilikuwa majira ya saa 7 za usiku wakati wimbo wa 'Ana' ukiwa hewani, ndipo kiongozi wa bendi ya Bogoss Musica Nyoshi El Saadat aliposikika akimkaribisha jukwaani muimbaji wa FM Academia, Mulemule.

"Humu ndani tunao mwanamuziki wenzetu, ambao niliwahi kufanya nao kazi Fm Academia na walishiriki kuimba wimbo huu wa Ana, tungependa kuwakaribisha washiriki nasi, Jose Mara na Mulemule popote mlipo tunawaomba mje hapa jukwaani tuwakumbushe mashabiki kile tulichofanya tukiwa bendi moja," alisema Nyoshi kabla ya mashabiki kushangilia kwa nguvu.

Jose Mara na Mulemule wakakwea jukwaa la Bogoss na kutupia masauti masauti yao watu wakasisimka na kuwatunza.

Baada ya kushuka jukwaani wanamuziki hao, Nyoshi hakuishia hapo, alisikika tena akimkalibisha  mwanamuziki Papii Kocha mtoto wa Nguza Viking.

"Leo shoo yetu imetembelewa na wanamuziki wengi sana wa bendi tofauti tofauti, hii inaonyesha ni upendo wa sisi wanamuziki na tunaomba tuendelee hivi hivi kupendana na kusaidiana kwenye kazi

"Sasa hivi namuita Papii Kocha aje awasalimie, huyu ni mwanangu kabisa katika kazi kama alivyo Jose Mara, na tuliwahi nae kuimba bendi ya FM Academia, Papii Kocha nakuomba uje hapa jukwaani,"alisikika Nyoshi akisema

Papii Kocha alipanda jukwaani na kuimba wimbo wa Seya alioimba na baba yake Nguza Viking.

Wimbo huo uliwaibua watu kwa kelele za furaha huku wakipishana mbele kwenda kumtunza Papii Kocha.

Papii Kocha alipoteremka jukwaani, Nyoshi alimpandisha Jimmy Manzaka ambaye aliwahi kupitia bendi kama Decca musica na Rufita na sasa atamba na Rhumba ya wimbo wa 'Coco Channel'.

Advertisement