Mashabiki wanawake walivyoipamba mechi ya Yanga, Simba

Muktasari:

Kwa sasa ukienda katika viwanja vya soka si ajabu kuona umati wa wasichana na wanawake wakiwa sehemu ya kuhanikiza, kuchagiza na kufanya ‘amsha amsha’ kwa ajili ya kuchochea ushindi ama wa klabu au wa timu ya taifa

Dar es Salaam. Kwa muda mrefu soka barani Afrika hasa hapa Tanzania lilitawaliwa na wanaume. Kuanzia uwanjani kwa wachezaji, viongozi, mashabiki na wadau wengine wa mchezo huo kwa zaidi ya asilimia 90 ilimilikiwa na jinsia hiyo.

Mbali na kutajwa kutumika kama kiunganishi na kichocheo kikubwa kwa matukio mbalimbali ya kitaifa kama harakati za kusaka uhuru, lakini bado soka lilikuwa likitawaliwa na wanaume pekee.

Yawezekana hilo lilitokana na mazingira, utamaduni wa jamii au mfumo dume uliotawala kwa muda mrefu, lakini sasa hali imebadilika kwa kiasi kikubwa.

Kwa sasa ukienda katika viwanja vya soka si ajabu kuona umati wa wasichana na wanawake wakiwa sehemu ya kuhanikiza, kuchagiza na kufanya ‘amsha amsha’ kwa ajili ya kuchochea ushindi ama wa klabu au wa timu ya taifa.

Sasa wanawake wamekuwa wakionyesha hisia na mapenzi kwa timu wanazoshabikia, hujitokeza kwa wingi viwanjani huku wakiwa katika mavazi yenye rangi za jezi za klabu zao. Wengine husafiri hadi mikoani na nje ya nchi kwa ajili ya kushabikia mchezo huo tu.

Mechi ya Simba na Yanga ni miongoni mwa mechi ambazo hukusanya sehemu kubwa ya wanawake katika uwanja inakopigwa mechi hiyo kama ile iliyochezwa juzi Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam pale Yanga walipoikaribisha Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Wanawake walikuwa sehemu ya hamasa kubwa katika mchezo huo ambapo kila upande mashabiki wake walifurika kuunga mkono timu yao bila kujali makundi yao katika jamii wakiwamo wasanii, wanasiasa, wanamuziki na hata wataalamu na wasomi wa kada mbalimbali.

Mchango wa wanawake uwajani

Msanii wa Bongo Movie na muziki, Ummy Wenceslaus ‘Dokii’ ni shabiki mkubwa wa klabu ya Yanga anasema amekuwa akipenda soka tangu alipokuwa mtoto mdogo.

“Familia yetu yote ni Yanga baba na mama mtu ambaye amenikataa ni mwanangu tu yeye ndiye anapenda Simba sijui amechukua wapi,” anasema Dokii ambaye ni Mtanzania anayependa kuongea lafudhi ya Kenya.

Anasema amekuwa shabiki wa mpira na haoni tabu kusimamisha shughuli zake kushabikia soka kwa sababu ni starehe yake.

“Ikitokea Yanga imefungwa huwa naumia na ikishinda hufurahi sana, lakini matokeo ya mchezo wa leo (juzi) tangu naanza safari kutoka nyumbani nilikuwa na wasiwasi kwa sababu Simba wako vizuri kwa sasa tofauti na Yanga. Nilikuja uwanjani kusaidia ushindi wa timu yangu,” anasema Dokii.

Hata hivyo, anasema kutokana na ubora wao, Simba walipaswa kuifunga Yanga mabao mengi lakini anafurahi kuona wamefungwa bao moja tu.

Pauline Chuma, mdau wa miaka mingi wa Yanga, ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha klabu yake hiyo yenye maskani yake Jangwani, Dar es Salaam anasema analojukumu kubwa kwa ajili ya mafanikio ya timu yake.

“Napenda soka na napenda Yanga kwa mapenzi yangu yote. Nipo Yanga kwa ajili ya kuitumikia na si initumikie. Sehemu ya mambo ninayofanya ndani ya klabu ni kusimama milangoni kwa ajili ya kusimamia mapato na shughuli nyingine nyingi za timu,” anasema Pauline na kukusitiza mapenzi kwa Yanga na mpira kwa ujumla ilitokea tu lakini baba na mama yake wako pembeni kabisa.

Anasema yeye ni mjasiriamali hivyo shughuli zake hazimbani kuiona timu yake: “Nafanya biashara ya jezi hata ninapokuwa nakuja uwanjani huwa nabeba na kuuza kabla ya mechi lakini mchezo unapoanza naziweka kwenye begi na kuangalia burudani na kushangilia kuchagiza ushindi”.

Licha ya kulala mbele ya mnyama kwa bao lililofungwa na Meddie Kagere, Pauline anasema hilo halimnyimi raha kwa kuwa ni sehemu ya mchezo.

“Matokeo yapo ya aina nyingi, ukiwa unalijua hilo kamwe haliwezi kukusumbua kikubwa ninachoomba kwa timu yangu watulie na wasikate tamaa,” anasema Pauline.

Alimpongeza Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera kutokana na namna anavyojitoa kwa ajili ya Yanga: “Ametukuta katika hali mbaya lakini amesimama imara”.

Kwa upande wake Naomi Mapunda aliyefika uwanjani hapo akiwa amevalia jezi ya Simba, anasema alianza kupenda soka tangu akiwa mtoto.

“Napenda mpira hasa timu yangu ya Simba, hii ni kama ambavyo watu wengine wanapenda muziki au kubeti. Kutokana na mapenzi niliyonayo huwa nasafiri mikoani kuifuata Simba inapocheza,” anasema Naomi ambaye ni mkazi wa Tabata Segerea, jijini Dar es Salaam.

Mrembo huyo anawataja baadhi ya wachezaji wanaomvutia ndani ya klabu ya Simba kuwa ni Mnyarwanda Meddie Kagere na Mzambia Cletus Chama.

Mrembo wa Simba kutoka Tawi la Ubungo Terminal, Sophia Hashim ambaye aliongozana na wenzake kutoka tawini hapo kwenda kuishangilia timu yao anasema, anapenda soka kupita kiasi.

“Huwa napanga muda wangu wa kustarehe kwa ajili ya soka tu. Nasafiri sehemu mbalimbali kwa ajili ya kuishangilia Simba ipate ushindi,” anasema Sophia. Anasema msimu huu timu yake ina kikosi kizuri na kipana, hivyo ana uhakika wa kuchukua makombe tofauti kama Ligi Kuu Bara na kufika mbali katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Simba ni timu yetu, huu ni mwaka wetu wa kufanya vizuri na pia kombe la Ligi Kuu ni letu,” anaeleza.

Wadau wazungumza

Mchezaji wa Coastal Union, Athuman Idd ‘Chuji’ ambaye amewahi kuzichezea Simba na Yanga kwa nyakati tofauti anasema: “Soka ni mchezo namba moja kwa kupendwa duniani, ndio maana ikawa rahisi kwa wanawake nao kuvutiwa”.

“Nafikiri utandawazi ndicho kitu cha kwanza kilichochangia kuongeza hamasa. Wanavyowaona wenzao Ulaya wanavyokwenda viwanjani na familia zao, wanavyoshangilia timu zao ndiyo maana na kwetu hamasa inaongezeka,” anasema Chuji ambaye anacheza nafasi ya kiungo.

Chuji anatoa wito kwa wanaoamini soka ni mpira wa kiume kuachana na dhana hiyo kwa kuwa mchezo huo ni wa kila mtu.

Beki wa kati wa Simba, Muivory Coast Pascal Wawa anasema: “Naona si kitu cha ajabu soka kupendwa na wanawake kwani ni mchezo kama ilivyo mingine hivyo wanawake kushabikia ni jambo la kawaida.

Kocha Msaidizi wa Timu wa Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’ Edna Lema anasema: “Soka kwa wanawake sasa ni asilimia 60 kwa 40 kulinganisha na wanaume. Wapo wanaoupenda kwa mapenzi tu na wengine kufuata wenzao kama marafiki”.

Wakati kwa Afrika hususan Afrika Mashariki, mwamko wa soka ukishika kasi sasa, barani Ulaya hususani Uingereza mchezo huo unapendwa na wanawake wengi ambao hufurika viwanjani kushuhudia mechi.

Nchini Hispania katika kila orodha ya mashabiki 20 maarufu wa klabu pendwa na kongwe duniani ya Real Madrid kuna wanawake watatu.