Katibu Dodoma Fc ajiuzulu kisa vipigo mfululizo

Muktasari:

Uamuzi wa katibu huyo umetokana na mwenendo mbovu wa timu hiyo msimu huu.

Dodoma. Kipigo cha nyumbani ilichopata Dodoma Fc kutoka kwa Polisi Tanzania jana Jumapili kimesababisha Katibu Mkuu wa timu hiyo Fortunato Johnson kuachia ngazi.

Jana Jumapili Dodoma Fc ilikubali kichapo cha mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma na kuwaacha mashabiki na watazamaji wa timu hiyo wakishangaa kilichotokea.

Baada ya mchezo huo, baadhi ya wadau wa timu hiyo walibaki uwanjani hapo wakiwa kwenye vikundi wakijadili hatma ya timu hiyo huku wengine wakishauri mabadiliko yafanyike ndani ya timu hiyo.

Mchana leo Katibu Mkuu Johnson amelazimika kuachia ngazi akidai anatimiza dhana ya uwajibikaji kwa matokeo mabaya inayopata timu hiyo.

Johnson amesema "binafsi nimeumizwa na matokeo mabovu ya jana, nimechukua muda mwingi kutafakari ni wapi tunapokosea kila mara tunajitahidi kuzipunguza bila kufanikiwa kwa kiwango tulichotarajia."

"Nawajibika Dodoma FC sio mali yangu binafsi ni mali ya watu wote wa Dodoma, nimetafakari kwa kina kila hatua tunayopitia, nimeona ni vema na haki kuwasiliana na viongozi wangu wakuu wa Klabu kuwaomba mimi niachie ngazi," alisema Johnson

Baada ya kutangaza hilo ameongeza kuwa ataendelea kuwa mdau na kuwa karibu na timu hiyo katika masuala endapo atashirikishwa.