Kha! Messi hachoki kufunga tu jamani

Muktasari:

Kufunga kulimfanya Messi awe amefikisha mabao 30 katika michuano yote aliyocheza msimu huu akiwa na Barcelona.

BARCELONA, HISPANIA. STAA wa Barcelona, Lionel Messi amezidi kuangusha rekodi moja baada ya nyingine huko Hispania.
Staa huyo juzi Jumamosi aliifungia Barca bao pekee kwenye mechi ya La Liga dhidi ya Valladolid, akiweka nyavuni kwa mkwaju wa penalti. Kufunga kulimfanya Messi awe amefikisha mabao 30 katika michuano yote aliyocheza msimu huu akiwa na Barcelona.
Kwa kufanya hivyo, staa huyo mshindi mara tano wa tuzo ya Ballon d'Or, ambaye atafikisha umri wa miaka 32 baadaye msimu huu, ameweka rekodi ya kufikisha mabao yanaoanzia 30 kwa misimu 11 mfululizo.
Bao lake liliifanya Barcelona pia kumaliza ukame wa kushinda baada ya kutoka kapa katika mechi tatu kabla ya kuwakaribisha Valladolid huko Camp Nou.
Penalti hiyo ilitokana na Gerard Pique kufanyiwa madhambi ndani ya boksi na Messi akapiga mkwaju na kufunga. Licha ya kwamba Messi alitoka kapa katika mechi mbili zilizopita, penalti hiyo ilikuwa bao lake la 13 katika mechi 13 za mwisho. Messi angeweza kufunga zaidi kama si penalti yake nyingine aliyopiga kwenye mechi hiyo dakika tano za mwisho kuokolewa.