Man United yaweka mzigo kwa Neymar

Muktasari:

Supastaa huyo wa Kibrazili amekuwa akiwindwa pia na Real Madrid pamoja na Barcelona wanaotaka kumrudisha kwenye kikosi chao

Paris,Ufaransa. Manchester United wameripotiwa kuandaa pesa ndefu, Pauni 262 milioni kumnasa fowadi wa Paris Saint-Germain, Neymar.
Mipango yote inawekwa sawa kuhakikisha dili hilo linakamilishwa katika dirisha lijalo la usajili wa majira ya kiangazi huko Ulaya.
Supastaa huyo wa Kibrazili amekuwa akiwindwa pia na Real Madrid pamoja na Barcelona wanaotaka kumrudisha kwenye kikosi chao baada ya kuwaacha miaka miwili iliyopita kwa ada ya Pauni 200 milioni.
Hata hivyo, rais wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu hivi karibuni alisema kwamba wanaona kwamba watakuwa kwenye wakati mgumu sana kumsajili tena mshambuliaji huyo, hivyo kuwafanya Man United kubaki kwenye vita ya wao wenyewe.
Real Madrid mpango wao wa kwanza ni kumsajili Eden Hazard na kama hilo litafanikiwa basi hawatangaika na Neymar na hivyo mchezaji huyo atawafanya Man United kuwa bize kwenye kuwashawishi PSG kumuuza.
Kwa mujibu wa Don Balon, kocha wa muda wa Man United, Ole Gunnar Solskjaer, ambaye anatarajia kupewa mikoba ya jumla kuinoa timu hiyo mwishoni mwa msimu, anamtaka Neymar kama staa atakayekuja kuifanya Man United kuwa na nguvu tena ya kutawala Ulaya.
Baada ya hapo kilichoelezwa ni kwamba wababe hao wa Old Trafford wapo tayari kuishtua dunia kwa kuweka mkwanja mrefu mezani kwa PSG, Pauni 262 milioni ili kufanya biashara.
Neymar amefunga mabao 105 katika mechi 186 alizoichezea Barcelona kati ya 2013 na 2017 kabla ya kuvunja rekodi ya dunia kwenye uhamisho alipohamia PSG katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka 2017.
Akiwa kwenye kikosi cha mabingwa hao wa Ufaransa, Mbrazili huyo amefunga mabao 48 katika mechi 53, lakini jina lake limekuwa halikauki kwenye tetesi kwamba anataka kuachana na wababe hao wa Ufaransa.
Wiki iliyopita, PSG waliichapa Man United 2-0 kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na Neymar hakucheza mechi hiyo kutokana na kuwa majeruhi.