NBA, FIBA kuanzisha ligi ya kikapu ya kulipwa Afrika

Monday February 18 2019

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Chama cha mpira wa kikapu Marekani (NBA) kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la mpira wa kikapu (FIBA) wametangaza kuanzisha Ligi ya kulipwa ya Mpira wa kikapu Afrika.

Mpango huo umekuja siku chache baada ya rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama ambaye ni shabiki wa mpira wa kikapu kushauri kuanzishwa kwa Ligi ya mchezo huo Afrika.

Baada ya ushauri huo wa rais Obama, FIBA na NBA Jumamosi iliyopita wametangaza rasmi kuanzishwa kwa Ligi hiyo iliyopewa jina la Basketball Africa League (BAL).

Taarifa ya FIBA na NBA ilifafanua kwamba, ligi hiyo itaanza mapema Januari, 2020 na itakuwa ikishishirikisha mataifa 12 ya bara la Afrika.

Hivi karibuni, rais mstaafu Obama alishauri kuanzishwa kwa Ligi hiyo akisisitiza kwamba itajenga timu bora ya kikapu huku akiweka wazi kuwa ni mpenzi mkubwa wa mchezo huo.

Kamishina wa NBA, Adam Silver alisema rais Obama ameonyesha hali ya kuwepo kwa ligi hiyo.

Katika video ambayo Obama anaonekana akisalimiana na wachezaji wa mpira wa kikapu wa NBA na wale wa Afrika, rais huyo mstaafu alivutiwa na vipaji vya wachezaji chipukizi huku akiwataka kuonyesha juhudi zaidi ili wafike mbali.

"Naamini na ninatumanini kupitia michezo kama mkiweka jitihada lazima mfanikiwe," alisema Obama.

Katibu Mkuu wa FIBA, Andreas Zagklis alisema ushirikiano wao na NBA kuanzisha ligi hiyo ni muendelezo wa walichokianza kwenye programu ya Basketball Without Borders (BWB) inayofanywa na FIBA Afrika.

"Ligi ya Afrika ni muhimu kwa kuendeleza mkakati wa maendeleo ya mpira wa kikapu Afrika, huo utakuwa muendelezo wa programu zetu katika bara hilo na itatengeneza fursa zaidi kwenye michezo," alisema Zagklis.

 

 

 

 

 

 

Advertisement