Mawenzi FC yatulizwa na Mlale, shabiki apigwa

Muktasari:

Katika msimamo wa kundi hilo, Namungo FC inaongoza kwa kukusanya pointi 28 huku Mbeya Kwanza FC ikiweka kibindo pointi 27 wakati Mlale FC ikiwa na pointi 25 na Mawenzi FC ikiwa na pointi 24.

Morogoro. Mawenzi FC imebanwa mbavu na Mlale FC baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 katika mchezo ligi daraja la kwanza uliopigwa jana kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Mawenzi FC ilipata bao la kuongoza dakika ya 78, lililofungwa na mshambuliaji Hassan Mbande kwa mkwaju wa penalti baada ya beki wa Mlale FC, Anthony Samsoli kumfanyia madhabi Joseph Mkosa na mwamuzi wa kati kutoka Tabora, Dachi Mabuyu kutoa adhabu hiyo.

Mlale FC ilisawazisha bao hilo kupitia mshambuliaji wake Iddy Gamba kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 81.

Katika mchezo huo, dakika ya 78 kiungo mshambuliaji wa Mawenzi Market FC, Joseph Mkosa alilazimika kutolewa nje ya uwanja baada ya kupoteza fahamu kufuatia kufanyiwa madhambi na beki wa Mlale FC, Anthony Samsoli.

Katika hatua nyingine shabiki wa Mawenzi Market FC, Juma Hamis amejikuta akiugulia maumivu baada ya kukumbana na kipigo kutoka kwa mashabiki wa Mlale FC.

Shabiki huyo alikumbana na kipigo hicho dakika chache baada ya mchezo huo kumalizika katika lango kuu la kutokea uwanja wa Jamhuri na kuumizwa sehemu ya kichwani.

Katika msimamo wa kundi hilo, Namungo FC inaongoza kwa kukusanya pointi 28 huku Mbeya Kwanza FC ikiweka kibindo pointi 27 wakati Mlale FC ikiwa na pointi 25 na Mawenzi FC ikiwa na pointi 24.