Amechoka Petit amponda Mesut Ozil, adai hana hamu na soka

Monday February 18 2019

 

London, England. Kuna nini kati ya Unai Emery na Mesut Ozil? Mashabiki wa soka wamekuwa wakijiuliza swali hilo baada ya Kocha wa Arsenal, Unai Emery kuendelea kumsugulisha benchi kiungo mahiri mchezeshaji wa timu hiyo, Mesut Ozil.

Ozil huku akiwa fiti aliachwa nyumbani London wakati Arsenal iliposafiri kwenda kucheza na BATE ugenini katika pambano la mtoano michuano ya Europa Alhamis iliyopita na endapo angecheza mechi hiyo ingekuwa ya 100 kwake katika maisha yake ya soka Arsenal.

Watu wanaishia kukisia tu kinachoendelea. Upande mwingine unamlaumu Emery na upande mwingine unamlaumu Ozil. Lakini staa wa zamani wa Arsenal, Emmanuel Petit ambaye zamani alilitendea haki dimba la Arsenal anadai anajua kinachoendelea.

Petit anadai Emery ambaye ni Mhispaniola hana tatizo lolote na staa huyo Mjerumani isipokuwa Ozil amekuwa hajitumia ndani na nje ya uwanja na amekosa kiu ya kupata mafanikio kitu ambacho kinamfanya Emery ampige benchi.

“Nina heshima kubwa kwa Ozil lakini Ozil ambaye nilipenda kumuona miaka michache iliyopita alikuwa mmoja kati ya viungo bora duniani na ilikuwa raha kumtazama. Sasa hivi hakuna hata raha kumtazama au kumuona katika timu kwa sababu amepoteza kiu,” alisema Petit.

“Ozil ni mchezaji mkubwa lakini sio mpambanaji. Haongei. Wakati mwingine anakuwa kama mzimu uwanjani. Hasemi chochote kwa wachezaji wenzake. Haonyeshi hisia zozote,” aliongeza Petit ambaye enzi zake alisifika kwa kombinesheni nzuri na staa mwingine wa zamani wa Arsenal, Patrick Vieira.

Kumekuwa na wasiwasi Kocha wa Arsenal, Unai Emery amekuwa na matatizo na wachezaji wenye majina makubwa tangu akiwa na PSG wakati alipojikuta katika matatizo na Neymar ambaye alitaka kukaa juu yake.

Hata hivyo, Petit anaamini tatizo la Emery kwa Neymar ni tofauti na tatizo la Ozil na anaamini wawili hao hawajakwaruzana isipokuwa Ozil ameshindwa kujituma katika kikosi cha kocha huyo.

“Kwangu ni rahisi tu. Baada ya Kombe la Dunia wote tunajua kwanini ilisemwa kuwa alicheza vibaya. Ni kwa sababu ya picha aliyopiga na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan. Lakini kabla ya hapo lini uliwahi kumuona Ozil anacheza vizuri sana uwanjani? Hata kabla ya Kombe la Dunia alikuwa anacheza mechi moja vizuri na nyingine tano vibaya. Ilikuwa hivi kwa miaka miwili iliyopita.

“Kwahiyo ilianza miaka miwili iliyopita kabla ya Kombe la Dunia. Kombe la Dunia kilikuwa kisu na kwa sababu ni mchezaji anayelipwa zaidi katika timu amekosa kiu na nadhani anasubiri kustaafu,” aliongeza Petit.

Habari kutoka ndani ya Arsenal zinadai Ozil aligoma kuondoka Arsenal katika dirisha la Januari huku PSG ikimtaka kwa uhamisho wa mkopo kutokana na kuumia kwa Neymar. Inasemekana Ozil hataki kwenda popote kwa uhamisho wa mkopo na badala yake anaweza kuondoka jumla kama kuna timu itaweza kumlipa mshahara wake mwishoni mwa msimu huu.

Ozil aliyesaini mkataba mpya na Arsenal miezi michache kabla ya kuondoka kwa Arsene Wenger analipwa mshahara kwa Pauni 350,000 kwa wiki na dau hilo linadaiwa kuikausha akaunti ya Arsenal huku ikishindwa kununua wachezaji kwa sasa na badala yake imemchukua Denis Suarez kutoka Barcelona kwa dili la mkopo.

Endapo Arsenal itashindwa kuondokana na Ozil mwishoni mwa msimu kuna uwezekano mkubwa ikaingia sokoni ikiwa na dau kiduchu la kununua wachezaji wakati huu Emery akiangalia uwezekano wa kukisuka upya kikosi chake.

Advertisement