Peter Tino:Kipigo Yanga wala hakijaninyong'onyesha

Muktasari:

Hiyo ni mechi ya pili kwa watani hao kucheza msimu huu ambapo mechi ya mzunguko wa kwanza timu hizo zilitoka suluhu, Simba ikiwa mwenyeji.

Dar es Salaam. Nyota wa zamani wa Yanga, Peter Tino amesema kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Simba wala hakijamnyong'onyesha kwani kiwango walichoonyesha Yanga ni kama wameshinda mchezo huo kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Tino mchezaji aliyeiongoza Taifa Stars kufuzu kucheza Afcon mwaka 1980 anasema hakutegemea kuiona Yanga ikicheza kwa kiwango bora katika mchezo wa jana.

"Kama kuna shabiki wa Yanga alitoka Taifa jana amekasirishwa na matokeo basi mnafiki, sidhani kama kuna shabiki huyo, kwani kwa kiwango cha mpira Yanga yetu licha ya udhaifu ilitulia na kucheza mpira.

"Pamoja na kuwa tumefungwa, nafsi yangu imejisikia raha kwa kiwango ambacho Yanga walicheza, nilitegemea mabao mengi tu, lakini Simba ilishindwa hata tungefungwa mabao 3-0 au zaidi, lakini Simba wameshindwa na kuambulia bao moja ambalo kwangu naona kama ni bahati tu," alisema Tino.

Alisema aliiona Yanga ikicheza tofauti kabisa na alivyotarajia kwani timu ilitulia na wachezaji walipambana kuhakikisha hawafungwi licha ya changamoto wanazopitia klabuni lakini walionyesha soka safi.

"Nilienda uwanjani, lakini sikuwa na matumaini ya kushinda, niliamini fika lazima tufungwe goli nyingi, ila imekuwa tofauti kabisa.

"Narudia tena, kama kuna shabiki wa Yanga aliyekuwa uwanjani na akatoka amekasirika kwa matokeo yale, basi mnafiki, tumefungwa kimchezo tu lakini kwa kiwango cha mpira tumekionyesha hatukuwa dhaifu kama tulivyokuwa tukibezwa kabla," alisema Tino mfungaji wa bao lililoipeleka Tanzania katika Afcon1980.