Zidane atakavyotua hapo Stamford Bridge

Muktasari:

Taarifa zinadai kwamba mabosi wa Chelsea wapo kwenye mazungumzo ndani ya wiki hii kujadili kama wafanye mabadiliko ya kumwondoa Mtaliano huyo kwenye kikosi chao.

London, England. Chelsea wanafikiria mpango wa kumnasa Zinedine Zidane kuja kuchukua nafasi ya Maurizio Sarri kabla ya msimu kumalizika.
Taarifa zinadai kwamba mabosi wa Chelsea wapo kwenye mazungumzo ndani ya wiki hii kujadili kama wafanye mabadiliko ya kumwondoa Mtaliano huyo kwenye kikosi chao.
Mashabiki wamemchenjia Sarri baada ya timu yao ya Chelsea kukumbana na kipigo cha mabao 6-0 kutoka kwa Manchester City kwenye Ligi Kuu England wikiendi iliyopita na kuwafanya kuporomoka kwenye msimamo hadi nafasi ya sita.
Kitu kinachowakera mashabiki kuhusu Sarri ni kitendo chake cha kung'ang'ania staili moja ya kiuchezaji hata kama inawagharimu na jinsi anavyomchukulia kinda mwenye kipaji Callum Hudson-Odoi. Kitu kingine wanamtaka kocha huyo amwondoa Jorginho kwenye kiungo ya kukaba na hapo amtumie N'Golo Kante.
Lakini, kama Zidane, aliyeshinda mataji matatu mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na kikosi cha Real Madrid, akiwasili Chelsea, anaweza kubadili hali ya mambo. Kama atatua Stamford Bridge sasa basi hatakuwa na jambo jingine zaidi ya kuwatumia tu wachezaji waliopo hadi hapo mwisho wa msimu atakaposajili wengine. Kocha Sarri yeye huwa anang'ang'ania fomesheni moja tu, 4-3-3 habadiliki, lakini Zidane alionyesha alipokuwa Madrid kwamba kubadilisha fomesheni ndio staili anayopenda.
Hivi ndivyo utakavyokuwa mtoko wa Zidane kama atakubali kutua Stamford Bridge kujaribu kuwaweka pazuri The Blues.

4-3-3
Zidane alipenda sana kutumia fomesheni ya 4-3-3 katika mechi nyingi alizoinoa Real Madrid. Staili hiyo pengine inaonekana kuwakwaza wachezaji wa Chelsea kwa sababu wameitumia kwa karibu msimu wote sasa. Lakini, Zidane akitua hapo, anaweza kutumia fomesheni hiyo yeye akibadili wachezaji, anawazi kubaki na mabeki wa kati walewale, huku upande wa kushoto akimbadili Marcos Alonso na kumtumia Emerson Palmieri. Chini ya Sarri, Emerson ameanza kwenye mechi moja tu ya Ligi Kuu England, lakini Zidane atamrudisha Kante katika eneo lake analolimudu, kiungo ya chini. Jorginho atabaki kikosini, lakini atacheza juu na Kante atacheza chini, kama alivyokuwa akiwatumia Casemiro na Luka Modric huko Real Madrid. Kinda Callum Hudson-Odoi anatazamiwa kupata nafasi kwenye kikosi na Pedro na Willian wao wataanzia benchi.

4-2-2-2
Hii ni fomesheni ambayo Zidane aliitumia sana kwenye kikosi chake cha Real Madrid mmoja wa viungo wake watatu matata, Modric, Casemiro na Toni Kroos atakuwa amekosekana. Fomesheni hiyo inakuwa na viungo wawili wa kukaba, ambao wanasimama mbele ya mabeki wa kati, hivyo kuwaruhusu wachezaji wanne waliopo mbele kuwa na kazi zaidi ya kushambulia kuliko kukaba. Katika fomesheni hiyo, Eden Hazard atabaki kwenye upande wake wa kushoto kama Cristiano Ronaldo alivyokuwa akitumika na Zidane. Kovacic atakuwapo kwenye timu, lakini Hudson-Odoi atakosa nafasi huku Loftus-Cheek akiingia kwenye ile safu ya viungo wawili wa kushambulia. Fomesheni hiyo inaweza kubadilika kwa haraka sana na kuwa 4-4-2 wanapokuwa na majukumu ya kujilinda zaidi hasa wanapocheza na timu inayotumia zaidi mashambulizi ya kupita pembeni.

4-3-1-2
Katika fomesheni hii, Zidane anaweza kumtumia Hazard kwenye namba 10. Hilo si eneo ambalo staa huyo amekuwa akicheza licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa kupiga pasi na macho ya kuliona vyema goli. Kutokana na kuwa na vitu hivyo, Zidane anaweza kumbadili Hazard na kumtua kwenye nafasi hiyo. Kocha Sarri kwa msimu huu amekuwa akimtumia Hazard kama namba 9 feki, lakini Zidane anakuja na mabadiliko kumjaribu Hazard kucheza kwenye namba 10. Mfumo huo utawafanya mabeki wa timu pinzani kuondoa mkazo kwa Higuain kwa sababu kwenye sehemu ole ya ushambuliaji atapangwa sambamba na mmoja kati ya Callum Hudson-Odoi, Pedro au Willian.

4-1-2-1-2
Hii ni fomesheni nyingine ambayo ilitumia sana na Zidane. Fomesheni hiyo rahisi sana inaweza kubadilika na kuwa diamond pale inapohitajika na kama ikiwa hivyo, basi wachezaji Kante na Loftus-Cheek watakuwa muhimu sana kwenye fomesheni hiyo. Kante hapo atakuwa ameachana kabisa na majukumu ya kushambulia kama Fernandinho anavyotumika huko Manchester City, ambapo anakuwa kama vile ni beki wa kati namba tatu ndani ya uwanja, huku mabeki wa pembeni, Emerson na Cesar Azpilicueta watasogea kwenye sehemu ya kiungo. Loftus-Cheek yeye hatakuwa na majukumu ya kurudi nyuma sana, hivyo kazi kubwa itakuwa kujiweka kwenye nafasi ya kuanzisha mashambulizi ya kushtukiza kwa haraka. Lakini, kwa Zidane, fomesheni yoyote atakayotumia, wachezaji Kepa Arrizabalaga, Azpilicueta, Antonio Rudiger, Luiz, Kante, Jorginho, Hazard na Higuain watakuwa na nafasi kubwa ya kuanza, wakati Hudson-Odoi, Pedro na Willian watabadilishana kama ilivyo kwa Kovacic, Loftus-Cheek na Barkley.