Huyu ndiye MK14 hakuachi, ukibisha waulize Yanga

Muktasari:

Hilo lilikuwa bao la tisa kwa Kagere katika Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini ni la 22 na kama utajumuisha na mechi moja ya kirafiki basi atakuwa na mabao 23 kwa mashindano yote akiichezea Simba tangu asajiliwe

Dar es Salaam.Kumthibiti Meddie Kagere kwa dakika 90 ni kazi sana. Waarabu wa Al Ahly wanajua hilo kwa alichowafanya Jumanne iliyopita tu. Unajua ilikuwaje? Mwarabu aliamini atapata sare kwenye Uwanja wa Taifa katika Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kuona dakika zinayoyoma.
Kumbe walisahau kama Kagere yupo uwanjani. Ile Paap dakika ya 64 tu akawaliza...Waarabu chali! Si ikafika jana Jumamosi, Yanga buana wamepambana weee...wakijua wametuliza Mnyama, wakajisahau pia kama Kagere bado yupo uwanjani.
Ghafla tu mwanangu mara huyoo akajitwisha dakika ya 71. Hakuna namna Ramadhani Kabwili akaokota mpira wavuni, hadithi ikaishia hapo. Simba Moja, Yanga Bila, Kisha watu wakakung'uta vumbi kurudi makwao, Simba wanacheka, Yanga wamenuna.
Huenda Yanga hawana hamu kabisa ya kulisikia jina la Kagere. Ndio, wana kila sababu, kwani alichowafanyia jana ni kama vile aliwatuliza kiaina baada ya zile kejeli na maneno mofumbofu wakati wa kusajiliwa kwake Msimbazi akitokea Gor Mahia ya Kenya.
Wakati wa usajili mwanzoni mwa msimu, Yanga walikuwa wakimkejeli Kagere kuwa ni babu a.k.a Mhenga, lakini kwa namna alivyowanyoosha huenda hawatathubutu kumuita jina hilo tena. Straika huyo Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, aliwanyamazisha mashabiki hao wa Yanga Jangwani baada ya kufunga bao pekee na la ushindi lililoipa Simba pointi tatu muhimu katika mechi hiyo ya 102 kwa michezo ya watani wa jadi katika ligi tangu 1965.
Kagere alifunga bao hilo dakika ya 71 kwa kichwa akiwa mbele ya mabeki wa Yanga, Abdallah Shaibu 'Ninja' na Paul Godfrey pamoja na kipa Ramadhani Kabwili ambaye alishindwa kabisa kuruka kuuzuia mpira huo usitinge nyavuni.
Nahodha John Bocco, alikimbia na mpira kutoka katikati na kumimina majalo ambaye kwa utulivu, Kagere aliruka peke yake na kuukwamisha kushoto mwa lango la Yanga na kuamsha shangwe na hoihoi zilizoanikiza kwenye Uwanja wa Taifa, uliopigwa pambano hilo la watani.
Hilo lilikuwa bao la tisa kwa Kagere katika Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini ni la 22 na kama utajumuisha na mechi moja ya kirafiki basi atakuwa na mabao 23 kwa mashindano yote akiichezea Simba tangu asajiliwe.
Utamu sasa ni kwamba baada ya kufunga bao hilo straika huyo asiyechoka na ambaye alipumzishwa dakika ya 90 ili kupisha Haruna Niyonzima, aliamua kushangilia kwa kunengua.
Hata wakati wa kutoka pia alirudia tena kwa kutembea kwa mikogo na madoido yaliyomchukiza beki wa Yanga Kelvin Yondani aliyeenda kumhimiza na kumtegea mguu naye kujiangusha, kitendo kilichomfanya mwamuzi Hans Mabena aliyelimudu pambano hilo licha ya kuwa mara yake ya kwanza kuwachezesha watani, kumpa kadi ya njano.
Lakini sasa kama hujui ni kwamba Kagere karibu kila shindano ambalo Simba imetia mguu, amekuwa akitupia kuanzia mechi za kirafiki hadi zile za mashindano mengine na hapa  chini Mwanaspoti limekuwekea mabao yake yote ili kuonyesha alivyo hatari katika kucheka na nyavu, yaani ukizubaa mbele yake hakuachi buana! Huyu ndiye Meddie Kagere a.k.a MK14 ambako kule Kenya mashabiki wa AFC Leopards wanamajua vilivyo.

LIGI KUU BARA (9)
v Prisons (1-0)
v Mbeya City (2-0)- Yote
v Mwadui FC (3-1)- Moja
v Ruvu Shooting (5-0)- Moja
v JKT Tanzania (2-0)- Yote
v Mwadui FC (3-0) - Moja
v Yanga (1-0)

KAGAME CUP 2018 (4)
v APR (2-1)- Moja
v Singida Utd (1-1)-
v JKU (1-0) Nusu Fainali
v Azam (1-2) Fainali

NGAO YA JAMII (1)
v Mtibwa Sugar (2-1)- Moja

MECHI YA KIRAFIKI (1)
v FCEKsaifa (3-1)- Moja

LIGI YA MABINGWA AFRIKA (6)
v Mbabane Swallows (4-1)- Moja
v Mbabane Swallows (4-0)- Moja
v Nkana FC (3-1)-Moja
v JS Saoura (3-0)- Mbili

KOMBE LA MAPINDUZI 2019 (2)
v Chipukizi (4-1)- Mawili